Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana
12 Machi 2026
Usiku wa kuamkia Alhamis, Ukraine ilishambulia ghala la mafuta kwa ndege zisizo na rubani lililopo katka jimbo la Krasnodar, kusini mwa Urusi. Mashambulio hayo yamesababisha moto katika ghala hilo. Taarifa kutoka kwenye mamlaka ya kanda hiyo zimesema hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ndege zisizo na rubani za Ukraine zipatazo 80 zilidakwa na kuharibiwa katika maeneo kadhaa ya Urusi kwenye mashambulio hayo ya usiku kucha.
Kwa upande wake Ukraine imesema msichana wa miaka 15 ameuawa katika mji wa Menska ulio eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na mashambulio ya Urusi. Mamlaka ya eneo hilo imesema wazazi wa msichana huyo wamejeruhiwa kwenye kadhaia hiyo na majengo mawili ya makazi yameharibiwa.
Mashambulio hayo yametokea wakati ambapo duru ya tatu ya mazungumzo ya pande tatu ikikatizwa kutokana na vita katika Mashariki ya Kati, licha ya Marekani kuzishinikiza Urusi na Ukraine zifikie makubaliano ya amani.
Mjumbe wa Rais wa Urusi Vladimir Putin ameeleza kwamba alihudhuria mkutano na wapatanishi wa Marekani, hapo siku Jumatano. Mazungumzo hayo ya kwanza kati ya Moscow na Washington ameyataja kuwa yalikuwa na tija.
Mjumbe huyo Kirill Dmitriev, amesema majadiliano hayo ya jijini Florida yamefanyika baada ya Marekani kuondoa vikwazo kadhaa vya mafuta ya Urusi vilivyowekwa kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine mnamo mwaka 2022. Marekani imesema imefanya hivyo kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta wakati ambapo eneo la Mashariki ya Kati linakumbwa na vita.
Mjumbe wa Urusi katika juhudi za upatanishi Kirill Dmitriev, amesema nchi nyingi, hasa Marekani, sasa zimeanza kuelewa vyema kwamba mafuta na gesi ya Urusi yana jukumu muhimu na la kimfumo katika kuhakikisha utulivu wa uchumi wa dunia.
Wakati huo huo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, atafanya mazungumzo kuhusu namna ya kuongeza shinikizo dhidi ya Urusi atakapokutana siku ya Ijumaa mjini Paris na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Rais wa Ufaransa ameserma kundi la mataifa saba yaliyoendelea kichumi (G7) limekataa kulegeza hatua za adhabu dhidi ya Urusi kuhusu uvamizi wake wa Ukraine.
Zelensky na Macron pia watajadili juhudi za kidiplomasia za kusimamisha vita, kati ya Urusi na Ukraine. Marekani imependekeza mazungumzo mapya ya pande tatu yafanyike wiki ijayo. Kulingana na Zelensky, mazungumzo hayo yanaweza kufanyika nchini Uswisi au nchini Uturuki.