Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana
13 Agosti 2024Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa, idara zake za ulinzi wa anga zimezidungua droni 12 kwenye eneo la Kursk lililovamiwa na Ukraine. Kufikia Jumatatu, Kyiv ilidai kuwa ilifanikiwa kuteka sehemu yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,000 katika eneo hilo .
Shirika la habari la Urusi RIA limeinukuu ofisi ya shirika la ujasusi la nchi hiyo likisema kuwa hatua zilizochukuliwa na Zelensky,kwa wanajeshi wake kuingia nchini humo zinatishia mvutano huo kuendelea nje ya Ukraine.
Katika hatua nyingine, Ukraine imesema droni 38 za Urusi zimefanya mashambulizi nchini humo usiku wa kuamkia Jumanne. Sambamba na droni hizo makombora mengine mawili yalitumika pia kushambulia. Kulingana na jeshi la anga la Ukraine kupitia ukurasa wake wa Telegram, lilifanikiwa kuzidungua droni 30 katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo.
Soma zaidi: Putin: Mashambulizi ya Ukraine hayatazima oparesheni yetu
Mamlaka katika eneo la Summy ambalo ni moja ya sehemu zilizoshambuliwa zimesema mtu mmoja amejeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo. Zimeongeza kuwa, bomba moja la gesi na umeme pia vimeathiriwa hali iliyosababisha baadhi ya wakaazi wa Summy kubaki bila umeme na gesi. Shambulio kwenye eneo hilo limeharibu pia jengo la hospitali, na magari kadhaa.
Maeneo mengine yaliyokabiliwa na mashambulizi hayo ni pamoja na Cheniv na Mykolaiv ambako kulingana na mamlaka husika miundombinu ya raia ililengwa. Hakuna taarifa kuhusu uwepo wa vifo au majeruhi katika maeneo hayo.
Mashambulizi ya Urusi ndani ya Ukraine yaongezeka ndani ya saa 24
Kulingana na jeshi la Ukraine, Urusi imeongeza mashambulizi ndani ya Ukraine hasa katika eneo la Pokrovsk mashariki mwa nchi hiyo katika kipindi cha saa 24.
Kutokana na mashambulizi hayo, Ukraine imetangaza kuzuia mienendo yoyote ya raia katika eneo la kilometa 20 kaskazini mashariki mwa mpaka wake na Urusi
Katika hatua nyingine, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia IEA limesema kuwa, wawakilishi wake walikagua madhara katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na Urusi lakini hawakufanikiwa kufahamu chanzo chamoto uliotokea mahali hapo mwishoni mwa juma.
Moscow na Kyiv zimekuwa zikituhumiana kwa kuanzisha moto kwenye kinu hicho kikubwa cha nyuklia kilicho Ukraine. Urusi inadai kuwa, Ukraine ilishambulia eneo hilo kwa droni na kusababisha moto huku Ukraine ikisisitiza kwamba kuna uwezekano mkubwa moto huo ulitokana na uzembe wa Urusi au mhalifu aliyefanya kitendo hicho kwa makusudi.