1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Ukraine zafikia makubaliano kuhusu biashara ya gesi

31 Oktoba 2014

Urusi na Ukraine zimfikia makubaliano yatakayohakikisha usambazaji wa gesi katika msimu wa baridi Ukraine na barani Ulaya na hivyo kufikisha ukingoni mashauriano kati ya pande hizo mbili yaliyosimamiwa na umoja wa Ulaya

Picha: picture-alliance/dpa/S. Kozlov

Rais wa halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amesema amefurahishwa na hatua hiyo kati ya Ukraine na Urusi ya kufikia makubaliano kuhusu biashara ya gesi kwani imeonyesha uwajibikaji wa kisiasa,ushirikiano na kuheshimu malengo ya kiuchumi yaliyotawala katika kufikia maamuzi hayo na kuthibitisha makubaliano hayo

Barrosso ameongeza kusema hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha usalama wa kuwepo nishati barani Ulaya na sasa hakuna sababu ya wakaazi wa Ulaya kuhofu kukumbwa na baridi kali wakati wa majira haya ya baridi.

Urusi na Ukraine zatatua mzozo wa deni

Urusi na Ukraine zilikubaliana kuhusu usambazaji huo wa gesi jana jioni baada ya mazungumzo ya siku mbili mfululizo mjini Brussels.Urusi haijaiuzia gesi Ukraine tangu mwezi Juni mwaka huu kufuatia mzozo wa deni la mabilioni ya dola ambayo Urusi ilitaka lililipwe kwanza kabla ya kuendelea kuisambazia Ukraine gesi zaidi.

Waziri wa nishati wa Urusi Alexander NovakPicha: Reuters/Francois Lenoir

Umoja wa Ulaya umekuwa na wasiwasi kuwa mzozo huo huenda ukaathiri pia usambazaji wa gesi barani Ulaya ambako msimu wa baridi kali umeanza. Kiasi kikubwa cha gesi inayotumika barani humo inatoka Urusi na inapitia Ukraine.

Kamishna wa tume ya nishati wa umoja wa Ulaya Guenther Ottinger amesema makubaliano hayo yatadumu hadi mwishoni mwa mwezi Machi mwaka ujao na Ukraine inatarajiwa kuilipa Urusi dola bilioni 1.45 kama sehemu ya deni katika siku chache zijazo na kiasi kingine cha dola bilioni 1.65 ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Urusi kwa upande wake inatarajiwa kutekeleza agizo la serikali la kupunguza bei ya gei kwa ajili ya Ukraine kwa dola 100 kwa kila mita mraba ya gesi inayoiuzia Ukraine. Oettinger amesema Umoja wa Ulaya hautoi hakikisho lolote kuwa Ukraine itatimiza malipo hayo lakini amesema umoja huo unashughulikia mpango mpya wa kuipa msaada wa kifedha Ukraine mwaka ujao ifikapo mwezi Februari au Machi mwakani.

Umoja wa Ulaya watoa hakikisho

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wamesema watahakikisha umoja wa Ulaya unatimiza wajibu wake katika kutekelezwa kwa mapatano hayo kati ya Urusi na Ukraine.

Kamishna wa nishati wa Umoja wa Ulaya Guenther OettingerPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/Yves Logghe

Taarifa kutoka kwa viongozi hao wawili imesema Hollande na Merkel walizungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Ukraine Petro Poroshenko jana jioni na wamepokea vyema kutiwa saini kwa makubaliano hayo.

Hollande na Merkel pia wametilia msisitizo haja ya kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine ambako waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanataka kujitenga kwa eneo hilo.

Viongozi hao wa Ufaransa na Ujerumani wamesema wanatumai pande zote mbili zitarejea katika meza ya mazungumzo hivi punde ili kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa tarehe tano Septemba mjini Minsk yanatekelezwa kikamilifu.

Mapigano yameendelea mashariki mwa Ukraine licha ya makubaliano hayo na yamesababisha vifo vya wanajeshi 160 wa Ukraine.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: Gakuba Daniel