1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Urusi na Ukraine zashambuliana usiku wa kuamkia leo

Sylvia Mwehozi
21 Septemba 2023

Urusi imeishambulia miji ya Ukraine kwa makombora usiku wa kuamkia leo na kuwajeruhi watu 18, kuharibu miundombinu ya umeme na kusababisha umeme kukatika.

Ukraine Kyiv
Maafisa wa kuzima moto wakifanya kazi kwenye eneo la makazi, lililoharibiwa wakati wa shambulio la kombora la Urusi huko Kyiv,Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Mamlaka za Ukraine zimedai kwamba makombora ya Urusi yameitikisa miji kadhaa ya Ukraine ukiwemo mji mkuu wa Kyiv, mapema leo asubuhi na kusababisha moto, kuwaua watu wawili na wengine kuangukiwa na vifusi.

Shambulizi hilo la Urusi ni kubwa katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja, na limetokea baada ya kuwepo kwa ripoti kwamba kulikuwa na hujuma katika kambi ya anga ya kijeshi ya Urusi ya Chkalovsk karibu na Moscow.

Shambulizi hilo limesababisha kukatika umeme kwa muda katika mikoa mitano ya Ukraine Magharibi, katikati na Mashariki na hivyo kurejesha kumbukumbu ya kampeni ya Urusi ya mashambulizi ya anga yaliyolenga miundombinu muhimu katika msimu uliopita wa majira ya baridi na kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme kwa raia wa Ukraine.

Maafisa wa kuzima moto wakipambana baada ya shambulio la UrusiPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Kamanda mkuu wa vikosi vya Ukraine Valeriy Zaluzhnyi, amesema jumla ya makombora 43 yalivurumushwa na Urusi usiku kucha lakini mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine imeweza kudondosha 36 kati ya hayo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Ihor Klymenko amesema watu wawili wamefariki mjini Kharkiv,mashariki mwa Ukraine. Mashambulizi pia yameripotiwa katika mji wa magharibi wa Lviv.

Mashambulizi hayo yanafanyika wakati rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuwasilisha "mfumo wa amani" na pia katika siku ya kimataifa ya amani.

Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Ama kwa upande mwingine, idara ya usalama ya Ukraine SBU na jeshi la wanamaji wameishambulia kambi ya anga ya Saky katika eneo linalokaliwa na Urusi la Crimea usiku kucha na kusababisha "uharibifu mkubwa". Jeshi la Urusi limedai kudungua ndege 19 za droni za Ukraine zilizoilenga Crimea na Bahari Nyeusi ingawa haikutoa maelezo zaidi juu ya uharibifu uliojitokeza.

Soma pia: Ukraine yasema imevunja ngome ya "adui" huko Bakhmut

Ukraine imezidisha mashambulizi yake katika eneo la Bahari Nyeusi na Crimea ambayo ilinyakuliwa na Urusi mwaka 2014. Kyiv ilisema kwamba wimbi la mashambulizi yake kuelekea Crimea wiki iliyopita yaliharibu meli mbili za doria za Urusi pamoja na mfumo wa ulinzi wa anga.

Jana pia Ukraine iliripoti kwamba vikosi vyake vilishambulia kamandi moja ya Urusi iliyoko karibu na Sevastopol huko Crimea.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW