Urusi: Shambulio la ndege ya Syria ni ‘uchokozi’
19 Juni 2017Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa maswala ya kigeni mjini Beijing nchini China,waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema shambulizi hilo na Marekani dhidi ya ndege ya jeshi la Syria huenda likazidisha mzozo nchini Syria na pia kuhatarisha vita dhidi ya ugaidi. Kisa hicho kimetokea wakati ambapo majeshi ya Syria yameimarisha mashambulizi yake dhidi ya wapiganaji wa IS kusini na magharibi mwa Raqqa, huku nalo jeshi la waasi wa Syria lijulikanlo kama Syria Democratic forces linaloungwa mkono na Marekani likiendeleza vita dhidi ya kundi kundi hilo la IS ndani ya mji wa Raqqa,ambao ndio ngome ya wapiganaji hao wa IS. Katika taarifa Marekani imesema ilichukua hatua za kujilinda baada ya majeshi hayo ya Syria kuangusha mabomu karibu na eneo linalosimamiwa na jeshi la waasi la Syria Democratic forces. Marekani pia iliweka wazi kuwa haiyalengi majeshi ya Syria au Urusi, na iwapo muungano wa vikosi vyake utahitajika kufanya mashambulizi ya kujilinda basi havitasita kuchukua hatua.
Marekani inaunga mkono magaidi
Hata hivyo kamanda wa jeshi la Syria amelitaja shambulizi hilo dhidi ya ndege ya Syria kama ushahidi wa jukumu la Marekani katika kuunga mkono wapiganaji wa IS.Jeshi la Syria limeonya kutokea madhara makubwa kufuatia shambulizi hilo, na kusisitiza kuwa vitendo kama hivyo havitalizuia kuendelea na harakati zake za kupiga vita makundi ya kigaidi na kurejesha amani na usalama kwa wa Syria wote.Saa chache kabla ya kuangushwa kwa ndege hiyo ya jeshi ya Syria, Marekani ilisema kuwa vikosi vinavyomuunga mkono rais wa Syria Bashar al-Assad viliwashambulia wanajeshi wa jeshi la waasi la Syria Democratic forces na baadhi yao kujeruhiwa. Mapema mwezi huu, Marekani iliangusha ndege isiyo na rubani ya serikali ya Syria, baada ya ndege hiyo kushambulia vikosi karibu na kivuko cha mpaka cha al-Tanf kwenye mpaka kati ya Syria na Iraq.Taarifa nyingine ni kuwa jeshi la Ukombozi la Iran limetoa onyo kali dhidi ya wapiganaji wa IS,na kusema mashambulizi yeyote dhidi ya Iran yatailazimisha kutumia nguvu zaidi.Tangazo hilo lilitolewa baada ya jeshi hilo la Iran kurusha makombora yaliyolenga kundi hilo la IS mashariki mwa Syria.
Mwandishi:Jane Nyingi/AP/AFP
Mhariri:Josephat Charo