1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi: Tutafanya biashara na Afrika kwa sarafu ya kikanda

Hawa Bihoga
27 Julai 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema, taifa lake linafanya jitihada kuepusha mzozo wa chakula duniani, licha ya hofu ya kujiondoa kwenye makubaliano ya usafirishaji nafaka kutoka Ukraine, kutasababisha uhaba wa chakula.

Russland-Afrika-Gipfel in Sotschi 2019
Picha: Valery Sharifulin/Tass/dpa/picture alliance

Putini amesema hayo katika mkutano wa siku mbili kati ya Urusi na viongozi wa Afrika, ambao umehudhuriwa na idadi ndogo ya wakuu wa nchi ikilinganishwa na mkutano uliopita wa mwaka 2019.

Putin ameonesha utayari wa Urusi kuendelea kutoa misaada ya kiutuhasa katika mataifa yenye uhitaji wa haraka.

Ameongeza kuwa wanachokitaka ni kuwepo kwa ushiriki kamilifu katika kujenga mifumo sawa ya usambazwaji wa rasilimali.

Soma pia:Mkutano wa kilele kati ya Urusi na Afrika wafunguliwa rasmi

Putin ambaye amewekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi baada ya uvamizi wake nchini Ukraine, amesisitiza kwamba Urusi bado inaweza kuchukua nafasi ya Ukraine katika usambazaji wa nafaka kwenye misingi ya kibiashara na kama ruzuku kwa mataifa yenye uhitaji.

Putin: Urusi ina mifumo ya kibenki salama 

Akijikita zaidi katika ajenda ya biashara amesema Moscow, ina nia ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na bara hilo lenye watu bilioni 1.3 na wanaweza kutumia sarafu ya kikanda katika kufikia malengo ya kibiashara.

Rais Vladimir Putin akiwa na baadhi ya viongozi wa Afrika kwenye mkutano wa kilelePicha: Pavel Bednyakov/POOL/AFP/Getty Images

"Tupo tayari kufanya kazi na nchi za Afrika ili kuendeleza miundombinu yenu ya kifedha," alisema kwenye hotuba yake ya ufunguzi.

Aliwaambia viongozi hao kwamba katika utendaji huo wa kibiashara wataunganisha taasisi za benki kwa mfumo wa usambazaji wa ujumbe wa fedhauliotenenezwa Urusi.

Soma pia:Urusi kuchukuwa nafasi ya Ukraine kupeleka ngano Afrika - Putin

Putun akifafanua mfumo huo amesema, utaruhusu malipo ya kuvuka mpaka kufanywa bila kujali baadhi ya mifumo iliyopo ya vikwazo vya Magharibi.

"Hii itasaidia kuongeza utulivu, kutabirika kwa usalama wa kubadilishana biashara kwa pande zote."

Umoja wa Afrika: Kwa sasa amani ni muhimu zaidi

Awali katika mkutano huo wa kilele Putin alisema yupo tayari kusafirisha kiasi cha tani 25,000- 50,000 za nafaka katika mataifa kadhaa ya Afrika yakiwemo Burkina Faso, Zimbabwe, Mali, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne ijayo.

Zimbabwe ambayo rais Putin alitumia muda kueleza namna ambavyo itapokea msaada huo, imesema inayo hazina ya kutosha ya chakula kwa watu wake.

Rais Emmerson Mnangagwa amewaambia waandishi wa habari kando na mkutano huo kwamba taifa lake lina uhakika wa chakula cha kutosha.

Mataifa ya Afrika ambayo mengi yameonesha kutoegemea upande wowote wa mzozo kati ya Urusi na Ukraine, huku baadhi yakihofia mbinyo wa kiuchumi kutoka kwa wafadhili wao mataifa ya magharibi, yamesisitiza amani.

Viongozi wa Afrika wataka kumaliza mzozo wa Ukraine

02:31

This browser does not support the video element.

Soma pia:Putin akutana na viongozi wa Afrika

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika  na rais wa Comoro Azali Assoumani amesema ujumbe wa kusitisha mapigano ndio muhimu kwa sasa kati ya Urusi na Ukraine.

"Leo, ni muhimu kupigania amani endelevu kati ya Urusi na Ukraine, na huo ndio ujumbe ambao Umoja wa Afrika na mimi binafs tunawasilisha." Alisema

"Ni kwa ujumbe huu tulipomtembelea Rais Zelensky huko Kyiv na sasa tunazungumza nawe Rais wa Urusi Putin."

Mkutano huo wa kilele utahitimishwa hapo kesho, unatarajiwa kuwa na maazimio ya pamoja kati ya Afrika na Urusi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW