1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Urusi: Ukraine imeshambulia kinu cha nyuklia Zaporizhzhia

Hawa Bihoga
8 Aprili 2024

Urusi imeishutumu Ukraine kwa kufanya mashambulizi katika kinu cha nyuklia inachokidhibiti cha Zaporizhzhia mara tatu, na kuyataka mataifa ya Magharibi kujibu dhidi ya hatua hiyo. Ukraine imekanusha shutuma hizo.

Askari wa jeshi la Urusi akilinda doria katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia.
Askari wa jeshi la Urusi akilinda doria katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, baada ya kuchukua udhibiti.Picha: Andrey Borodulin/AFP

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA ambalo linawataalamu katika kinu hicho limesema kuwa ni mara ya kwanza  kwa kinu hicho ambacho ni kikubwa zaidi barani Ulaya kulengwa moja kwa moja tangu mwaka 2022 na kuongeza kuwa shambulio hilo linahatarisha usalama wa nyuklia.

Mkuu wa shirika hilo Rafael Grossi amesema kuwa wataalamu wake wamethibitisha mashambulizi matatu ya ndege zisizokuwa na rubani na kuwashutumu wanajeshi wa Urusi kuhusika na shambulio hilo.

Aidha ameonya juu ya ongezeko la hatari ya usalama inayokizonga kinu hicho cha nyuklia mbacho kilishuhudia mashambulizi makubwa wakati Urusi ikitaka kutwaa udhibiti katika eneo hilo la kimkakati.

Soma pia:Mashambulizi ya Urusi katika jimbo la Zaporizhzhia nchini Ukraine yawauawa watu watatu

Mkuu huyo wa IAEA amezionya pande zote kuheshimu kile alichokitaja kanuni katika kulinda usalama wa eneo hilo na kuongeza kuwa mashambulizi hayo ya kizembe yanaweza kuongeza hatari kubwa ya nyuklia na kutaka yakomeshwe mara moja.

"Tunazo kanuni zetu tano za msingi: Usishambulie mtambo, usishambulie kutokea kwenye mtambo, na msifanye mtambo kuwa kambi ya kijeshi, wala msikate ugavi wa umeme...Haya ndio mambo ya msingi ambayo lazima yazingatiwe." Alisema Mkuu huyo wa IAEA.

Urusi na Ukraine zimeendelea kushutumiana

Vikosi vya Urusi vilichukua udhiiti wa kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia mnamo 2022 muda mfupi baada ya uvamizi kamili kwa Ukraine.

Mtaalamu wa Shirika la Kimataia IAEA akifanya ukaguzi katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia, Ukraine- kinachodhibitiwa na UrusiPicha: IAEA Handout/REUTERS

Moscow na kyiv mara kadhaa zimekuwa zikishutumiana na kuhatarisha usalama wa nyuklia kwa kutekeleza mashambulizi katika kinu hicho.

Shirika la kushughulikia masuala ya nyuklia Urusi Rosatam limeishutumu Ukraine kwa kutekeleza mashambulizi hayo ikitumia ndege zisizo na rubani dhidi ya kinu hicho hapo jana Jumapili na kujeruhi watu watatu, lakini hakuna madhara ya mionzi ambayo yametajwa hadi sasa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Urusi Maria Zakharova amewataka viongozi wa dunia kulaani shambulio hilo alilolitaja kuwa ni la kigaidi.

Katika tamko lake Zakharova amehoji kuwa ni mara ngapi Ukraine ingelihatarisha usalama wa nyuklia katika mtambo huo kabla ya vuiongozi wa dunia kuchukua hatua?

Soma pia:IAEA yalaani mashambulizi ya Ukraine kwenye kinu cha nyuklia

Hata hivyo mamlaka nchini Ukraine imesema haihusiki dhidi ya shambulio katika mtambo huo wa nyuklia barani Ulaya, huku akisema shambulio hilo limetekelezwa kikamilifu na vikosi vya Urusi.

"Mashambulizi ya Urusi katika eneo la mtambo wa nyuklia Ukraine yamekuwa ni ya kujirudua mara kwa mara na linajulikana hilo, ikiwa kama mhalifu na mvamizi." Alisema msemaji wa Kurugenzi Kuu ya Ujasusi Ukraine, Andriy Usov.

Urusi yaendeleza mashambulizi Ukraine ikilenga miundombinu

Katika hatua nyingine Urusi imeendeleza mashambulizi yake ya anga ambapo usiku wa kuamkia leo imevurumisha droni kadhaa ambazo zimeshambulia miundombinu muhimu katika mkoa wa Zhytomyr.

Kufuatia shambulio hilo Mamlaka ya mji imewataka wakaazi kuendelea kusalia majumbani mwao wakiwa wamefunga madirisha kwa kile ilichokisema uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa, huku ikisisitiza shambulio hilo halikuleta madhara kwa raia.

Jeshi la anga la Ukraine limesema limedungua droni 17 aina sha Shahed  ambazo zinatumiwa na Urusi katika mashambulizi yake kwenye mikoa kadhaa ikiwemo Odesa,Mykolaiv na Zhytomyr.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Soma pia:Zelensky aliomba bunge la Marekani kuidhinisha msaada wa nchi yake

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, ameendelea kuwasisitiza washirika wake wa Magharibi kuendelea kupeleka msaada wa kijeshi kwa nchi yake kwani bila msaada huo itakuwa vigumu kwa vikosi vyake kufanikisha katika uwanja wa vita.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW