Urusi, Ukraine zaendelea kukabiliana vikali Kursk
8 Januari 2025Kwa mujibu wa mkuu wa majeshi wa Ukraine, siku ya Jumanne (Januari 7) kulitokea makabiliano 218 kwenye maeneo yote ya mstari wa mbele ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, ambapo kwenye mkoa wa Kursk pekee jeshi hilo limekabiliana na mashambulizi 94 ya Urusi.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, kamandi ya kikosi maalum cha Ukraine ilichapisha taarifa kwamba wanajeshi 13 wa Korea Kaskazini waliuawa, ingawa shirika la habari la Ujerumani (dpa) lilishindwa kuthibitisha taarifa hiyo kupitia vyanzo huru.
Soma zaidi: Ukraine yaanzisha oparesheni mpya ya kijeshi Kursk
Mnamo mwishoni mwa wiki, Kiev ilianzisha tena uvamizi wa kushitukiza kwenye mkoa huo ulio magharibi mwa Urusi, ambapo kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Vita ya Marekani (ISW), vikosi vya Ukraine vimesonga mbele kuelekea kaskazini mashariki mwa mji wa Sudzha.
ISW imesema hatua hiyo inaashiria kuwapo kwa operesheni iliyopangwa kwenye mkoa huo na pia matayarisho ya mashambulizi kwenye maeneo mengine ya mstari wa mbele, ikinukuu taarifa za data kutoka picha zilizochapishwa mtandaoni.
Urusi yakiri makabiliano na Ukraine
Wizara ya Ulinzi ya Urusi pamoja na waandishi wa blogu za kijeshi wameeleza kwamba vikosi vya Urusi vilikuwa vimekabiliana wanajeshi wa Ukraine kwenye maeneo kadhaa ya mkoa wa Kursk.
Kwa mara ya kwanza, vikosi vya Ukraine vilivuuka mpaka wa nchi hizo mbili mwezi Agosti mwaka jana na tangu wakati huo kuukalia mkoa wa Kursk, lakini kufuatia miezi kadhaa ya mapigano, jeshi la Urusi limerejesha takribani nusu ya eneo hilo mikononi mwake.
Soma zaidi: Vikosi vya kijeshi vya Ukraine na Urusi vyaendelea kushambuliana
Kupitia makubaliano yake na Pyongyang, Moscow inawatuma wanajeshi wa Korea Kaskazini kuvisaidia vikosi vyake kwenye mkoa huo, wakati Ukraine ikijaribu kupambana na uvamizi wa Urusi ulioanza tangu Februari 2022.
Wachambuzi wa kijeshi wanasema kwa Kiev kuanzisha mashambulizi ndani ya ardhi ya Urusi ni kuifanya Moscow kupoteza mwelekeo ndani ya Ukraine.