1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Droni 60 na maroketi 90 ya Urusi yaishambulia Ukraine

22 Machi 2024

Wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya wakikubaliana kutumia mali za Urusi zilizowekewa vikwazo kuisaidia Ukraine, Leo Urusi imefanya shambulizi katika eneo la mtambo mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme na kuua watano

Russia Ukraine War
Mtambo mkubwa wa umeme nchini Ukraine leo umeshambuliwa na Urusi na kusababisha kukatika kwa umeme nchini humoPicha: Denys Shmyha/Telegram/AP/picture alliance

Wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya mwanzoni mwa wiki hii wakikubaliana kutumia mali za Urusi zilizowekewa vikwazo kuisaidia Ukraine, Urusi yenyewe imeendeleza mashambulizi yake nchini Ukraine, hii leo imefanya shambulizi kubwa zaidi katika eneo lenye mtambo mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme na kusababisha kukatika kwa umeme na kuwaua watu wengine watano.

Soma zaidi. Urusi yafanya mashambulizi makali ya makombora nchini Ukraine

Taarifa iliyotolewa na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky imesema kuwa droni 60 zisizo na rubani na takriban maroketi 90 yametumiwa na Urusi kufanya shambulizi hilo hii leo.

Mamlaka nchini Ukraine imearifu kuwa shambulio la leo ni kubwa zaidi kwa miundombinu ya nishati ya Ukraine na moja ya shambulio kubwa zaidi tangu kuzuka kwa vita.

Moto mkubwa katika eneo la mtambo wa kuzalisha umeme nchini Ukraine ulioshambuliwa leo na UrusiPicha: Petro Andryuschenko/Telegram/AP/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Mkuu wa shirika la nishati la Ukraine, Volodymyr Kudrytskyi ameelezea shambulizi hilo la Urusi kwenye miundombinu ya nishati kuwa ni la makusudi na hata msimu uliopita wa baridi Urusi ilifanya hivyo ingawa sio kwa ukubwa kama shambulizi lilofanyika leo.

Soma zaidi. Watu watatu wauawa kufuatia mashambulizi ya Urusi katika miji ya Kherson na Donetsk

Akizungumzia haja ya kuwepo kwa ulinzi bora wa anga kwa njia ya video kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, Rais wa UKraine Volodymyr Zelenskyy ameendelea kusisitiza kupatiwa msaada zaidi wa silaha. "Ulinzi wote wa anga unaotolewa  kwa Ukraine, haswa na nchi za Ulaya, huweka miji na vijiji vyetu hai. Lakini mifumo iliyopo ya ulinzi wa anga haitoshi kulinda eneo letu lote dhidi ya ugaidi wa Urusi. Na sio suala la kuwepo kwa mamia ya mifumo, lakini kwa idadi inayoweza kufikiwa kulinda eneo lote la Ukraine."

Urusi: Tunaionya EU

Pamoja na shambulio hilo kutajwa kuwa ni kubwa zaidi bado Urusi imeahidi kuendeleza mashambulizi katika maeneo ya mipakani ya Ukraine.

Mapema leo, Msemaji wa Kremlin,Dmitry Peskovameuonya Umoja wa Ulaya katika mipango yake ya kutumia faida ya mauzo yake ya nafaka zake zinazouzwa nje na kutumia mali za Urusi zilizowekewa vikwazo kuisaidia Ukraine.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov ameuonya Umoja wa Ulaya katika mipango yake ya kutumia faida ya mauzo yake ya nafaka zake zinazouzwa nje na kutumia mali za Urusi zilizowekewa vikwazo kuisaidia UkrainePicha: Elena Palm/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Wakati hayo yakijiri, mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya Jamhuri ya Czech, Poland, Hungary na Slovakia wamekutana hii leo mjini Prague kujadili mpango wa Czech wa kuipatia silaha Ukraine.

Soma zaidi. Viongozi wa Ulaya wakubali kufungua mazungumzo na Bosnia juu ya kujiunga na EU

Akiuelezea mpango huo, Waziri wa mambo ya nje wa Poland Radoslaw Sikorski ambaye pia amehudhuria kikao hicho amasema "Nimalizie kwa kuipongeza na kuishukuru Jamhuri ya Czech na kila mtu aliyechangia kuwa na wazo hili zuri la mpango wa risasi. Tunayo furaha kubwa kuchangia, sio tu kifedha, lakini kwa operesheni bora ya vifaa ili risasi ziweze  kufika pale zinapohitajika .Nina furaha pia kwamba tumethibitisha yale ambayo nchi zetu zilitangaza hapo awali kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa''.

Itakumbukwa kuwa Ukraine imekuwa ikitoa wito wa mara kwa mara wa kupata msaada wa silaha za kisasa kutoka kwa mataifa ya mgaharibi ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi.


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW