Urusi yaahidi kulisaidia kikamilifu bara la Afrika
10 Novemba 2024Rais wa Urusi Vladmir Putin ameahidi kutowa msaada kamili kwa bara la Afrika.
Ahadi hiyo imetolewa leo Jumapili katika mkutano kati ya maafisa wa bara la Afrika na Urusi huko Sochi, Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.
Katika hotuba ya rais Putin iliyotolewa na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov mbele ya mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa mengine pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu, kiongozi huyo amesema nchi yake itaendelea kuzisaidia kikamilifu nchi washirika wake barani Afrika katika sekta mbali mbali.
Amesema Urusi inaweza kuyasaidia mataifa hayo ya Afrika katika maendeleo endelevu, kupambana na ugaidi na itikadi kali pamoja na kupambana na majanga, matatizo ya chakula na athari zizanosababishwa na majanga ya kiasili.
Soma pia: Mkutano wa BRICS wamalizika kwa mataifa kutaka ushirikiano wa maslahi ya pande zoteMkutano huo wa Sochi kati ya Afrika na Urusi wa Jumamosi na Jumapili unakuja baada ya kufanyika mikutano miwili ya kilele kati ya pande hizo mbili iliyofanyika mwaka 2019 na 2023.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Lavrov amesema mahusiano ya nchi hiyo na Afrika yamekuwa yakiiendelea kuimarika zaidi akitilia mkazo kwamba hatua zimepigwa katika nyanja zote za mashirikiano.
Malengo ya Urusi
Mkutano huu pia ni fursa nyingine kwa Urusi kutangaza malengo yake ya kutaka kuona ulimwengu usioendeshwa na taifa au upande mmoja tu wa dunia,ikiwa ni baada ya taifa hilo kuaandaa mkutano wa kilele wa mataifa yanayokuwa kiuchumi ya BRICS.
Soma pia: Baerbock: Urusi inaendelea kutengwa na Jumuiya ya KimataifaUrusi inataka kuuonesha ulimwengu wa nchi za Magharibi kwamba vikwazo vyake vilivyolenga kuifanya itengwe kutokana na kuivamia Ukraine vimeshindwa kufanya kazi.
Kadhalika Urusi ilikuwa ina dhima kubwa barani Afrika katika enzi za Muungano wa Sovieti na imekuwa ikiuimarisha ushawishi wake katika bara hilo katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo kwa kupitia msaada wa makundi ya mamluki ya nchi hiyo pamoja na kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya rasilimali za mataifa ya bara hilo.