1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yaviamuru vikosi vyake kuondoka mji wa Kherson

10 Novemba 2022

Urusi imeviamuru vikosi vyake kujiondoa kutoka mji wa Kherson nchini Ukraine, ambao ndiyo mji mkuu pekee wa mkoa uliotekwa na majeshi Rais Vladmir Putin tangu kuanza kwa vita hivyo vilivyodumu kwa miezi nane sasa.

Ukraine Armee rückt weiter vor
Picha: Anatolii Stepanov/AFP/Getty Images

Tangazo hilo la Jumatano, limefuatia wiki kadhaa za kusonga mbele kwa vikosi vya Ukraine kuelekea mji wa Kherson na linaashiria pigo kubwa kwa kampeni ya kijeshi ya urusi nchini Ukraine, ambayo iliivamia mwishoni mwa mwezi Februari.

Katika maelezo yaliotangazwa kupitia televisheni, kamanda wa jeshi la Urusi nchini Ukraine, Jenerali Sergei Surovikin, alisema kuwa haiwezekani tena kufikisha mahitaji mjini Kherson, na kupendekeza badala yake waimarishe safu yao kwenye kingo ya kushoto ya mto Dnieper.

Soma pia: Putin 'sio mshukiwa pekee' katika uhalifu nchini Ukraine

"Nafahamu kuwa huu ni uamuzi mgumu sana, lakini wakati huo huo, tutahifadhi jambo muhimu zaidi - maisha ya wanajeshi wetu, na  kwa ujumla, ufanisi wa kimapambano wa askari, jambo ambalo halina faida kuimarisha eneo dogo la ukingo wa kulia," alisema Jenerali Surovikin.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu pia aliunga mkono maelezo hayo na kusema, "nakubaliana na mahitimisho yako na mapenedekezo. Endelea na uondoaji wa vikosi na kuchukua hatua zote kuvusha wanajeshi mto."

Mkuu wa jeshi la Urusi nchini Ukraine, Jenerali Sergei Surovikin.Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Tangazo hilo pia lilikuja saa kadhaa baada ya naibu kiongozi wa Kherson aliewekwa na Urusi, kuripotiwa kuuawa katika ajali ya gari, wiki kadhaa baada ya kuwasihi wakaazi kuondoka katika eneo hilo.

Kyiv yatilia mashaka, waunagaji wapaka mafuta

Lakini maafisa mjini Kyiv walijibu kwa tahadhari, wakisema jeshi la Urusi halina uwezekano wa kuondoka kutoka mji huo wa kimkakati bila mapigano, huku rais wa Marekani Joe Biden, akisema kujiondoa kwa Urusi ni ushahidi kwamba Moscow inakabiliwa na matatizo ya kweli kwenye uwanja wa mapambano.

Lakini mchambuzi wa kijeshi na ulinzi wa Urusi mwenye makao yake mjini Moscow, Pavel Felgenhauer, alisema tangazo hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Moscow, hatua iliyomsababishia ukosoaji mkubwa kwenye chaneli za Telegram zenye mafungamano na mrengo mkali wa kulia.

Waungaji mkono mashuhuri wa Kremlin akiwemo mwanzilishi wa kundi la mamluki wa kijeshi la Wagner Yevgeny Prigozhin, na mhariri mkuu wa shirika la habari la serikali la RT, Margarita Simonyan, walijaribu kulipaka mafuta tangazo la Surovikin, wakibainisha haja ya kunusuru maisha.

Soma pia: Vikosi vya Ukraine vyakomboa makaazi 40 ya Kherson

Kherson ni mmoja ya mikoa minne ya Ukraine ambayo rais Putin alitangaza mwezi Septemba kuiunganisha milele na Urusi, baada ya kura ya maoni iliyokoselewa kuwa haramu na Ukraine na washirika wake.

Hata hivyo kumekuwa na uvumi unaozidi katika wiki za karibuni kwamba Moscow huenda ama ikaondoka wanajeshi kutoka ukingo wa magharibi wa Mto Dnieper au kujichimbia kujiandaa na vita kali.

Kirill Stremousov, naibu mkuu wa utawala uliowekwa na Urusi mkoani Kherson, anaripotiwa kufariki katika ajali ya gari.Picha: AFP/Getty Images

Mapema Jumatano, daraja kuu lililoko kwenye barabara ya kutoka mji wa Kherson lililipuliwa, huku uvumi ukienea miongoni mwa wa Ukraine kwamba limelipuliwa na majeshi ya Urusi katika maandalizi ya kujiondoa.

Marekani yasema zaidi ya wanajeshi 100,000 wa Urusi wameuawa au kujeruhiwa

Katika hatua nyingine, mkuu wa majeshi ya Marekani Jenerali Mark Milley, amesema zaidi ya wanajeshi 100,000 wa Urusi wameuawa au kujeruhiwa nchini Ukraine, na kuongeza kuwa ni dhahiri hata Ukraine imepata hasara sawa na hiyo.

"Unatazamia zaidi ya wanajeshi 100,000 waliouawa au kujeruhiwa," Milley alisema katika matamshi kwenye Klabu ya Uchumi ya New York. Jambo sawa yumkini kwa upande wa Ukraine."

Takwimu zilizotolewa na Milley - ambazo hazikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru -- ndiyo za karibuni zaidi kutoka serikali ya Marekani, zaidi ya miezi nane tangu kuanza kwa vita hivyo.

Milley pia alisema kuna nafasi ya mazungumzo ya kumaliza vita, na kwamba ushindi wa kijeshi huenda usiwezekane kwa ama Urusi au Ukraine.

Soma pia: Zelensky avitaka vikosi vya Urusi viondoke Kherson

Putin kutohudhuria mkutano wa kilele wa G20

Wakati huo huo ikulu ya Kremlin imetangaza kuwa Rais Putin hatohudhuria mkutano wa kilele wa mataifa ya G20 mjini Bali Indonesia, na badala yake atawakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov.

Urusi yaendelea kushambulia miji ya Ukraine kwa makombora

01:44

This browser does not support the video element.

"Naweza kuthibitisha (waziri wa mambo ya nje) Sergei Lavrov ataongoza ujumbe wa Urusi kwenye mkutano wa G20. Programu ya Rais Putin bado inafanyiwa kazi, huenda akashiriki kwa njia ya mtandao," alisema Yulia Tomskaya, mkuu wa itifaki wa ubalozi wa Urusi nchini Indonesia.

Rais wa Marekani Joe Biden ambaye amemuita Putin "mhalifu wa kivita" na atahudhuria mkutano huo, alisema huko nyuma kwamba hakuwa na mpango wa kukutana na Putin mjini Bali endapo angeenda.

Rais wa Indonesia Joko Widogo alikuwa amemualika Putin kuhudhuria mkutano huo wa tarehe 15 -16 mwezi huu, lakini Kremlin haijathibitisha mipango ya kiongozi huyo mpaka sasa.

Chanzo: mashirika