Urusi yaanza kutoa chanjo ya Covid 19
5 Desemba 2020"Raia walio kwenye kundi lililo katika hatari kubwa ambao katikati ya kazi zao wanakutana na waathirika wengi wa virusi hivyo wanaweza kupewa chanjo hiyo," walisema maafisa.
Siku ya Jumamosi maafisa wa afya mjini Moscow walisema watakaopewa chanjo hiyo katika awamu hii ya kwanza ni watu wasiozidi umri wa miaka 60 tu huku watu wenye magonjwa mengine hatari, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha watoto wakiwekwa nje ya kundi la watakaopewa chanjo.
Meya wa Moscow Sergei Sobyanin ameandika katika tovuti yake binafsi, "katika saa tano zilizopita watu 5,000 wamejisajili kwa chanjo hiyo, walimu, madaktari, wafanyakazi wa jamii na wale ambao leo hii wanayahatarisha maisha yao zaidi."
Urusi haijaweka vikwazo vyovyote vya kitaifa kama nchi zengine Ulaya
Utoaji huu mkubwa wa chanjo umeanza wakati ambapo Urusi imeweka rekodi ya maambukizi ya siku moja ambapo jumla ya watu 28,782 wameripotiwa kuambukizwa na kupelekea idadi jumla ya maambukizi kufikia 2, 431, 731 tangu kuanza kwa janga hilo la virusi vya corona, hii ikiwa ni idadi ya nne kubwa zaidi duniani.
Licha ya ongezeko la maambukizi, Urusi haijaweka vikwazo kote nchini humo, vikwazo ambavyo vimewekwa katika sehemu zengine za Ulaya, ingawa baadhi ya sehemu nchini humo zimewekwa vikwazo. Urusi badala yake imeweka matumaini yake ya kuvidhibiti virusi vya corona katika chanjo. Rais Vladimir Putin siku ya Jumatano aliwaambia maafisa wa afya kuanza utoaji chanjo kwa kiasi kikubwa wiki ijayo akiongeza kwamba Urusi ina dozi karibu milioni mbili za chanjo ya Sputnik V.
Urusi ina chanjo mbili za Covid 19
Mwezi uliopita wizara ya ulinzi ya Urusi ilitangaza kampeni kubwa ya utoaji chanjo imeanzishwa katika jeshi la nchi hiyo na wanalenga kuwapa chanjo wanajeshi 400,000 namwishoni mwa mwaka huu wanatarajia kuwapa chanjo wanajeshi 80,000.
Urusi ina chanjo mbili za Covid 19, Sputnik V na nyengine ya Taasisi ya Siberia huku majaribio ya chanjo zote hizo yakiwa bado hayajakamilishwa. Chanjo hiyo ya Sputnik V inatolewa mara mbili ambapo mtu anadungwa sindano ya pili siku ishirini na moja baada ya kudungwa sindano ya kwanza.
Wanasayansi wameelezea hofu yao kuhusiana na kasi ambayo Urusi imetumia kuidhinisha matumizi ya chanjo yake kabla kukamilika kwa majaribio ya usalama wake.