1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yaanza luteka kubwa za jeshi lake la wanamaji

30 Julai 2024

Urusi imeanza luteka kubwa za kijeshi zinazohusisha sehemu zote za jeshi lake la wanamaji ambazo hazihusiki na mashambulizi yake nchini Ukraine . Haya ni kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya nchi hiyo.

Nyambizi ya Urusi yashiriki katika luteka ya kijeshi ya jeshi la wanamaji la nchi hiyo inayofanyika katika bahari za Arctic, Pasifiki, Baltic na Caspian mnamo Julai 30
Nyambizi ya Urusi yashiriki katika luteka ya kijeshi ya jeshi la wanamaji la nchi hiyoPicha: SNA/IMAGO

Meli zipatazo 300, zikiwemo nyambizi, na zaidi ya maafisa 20,000 watahusika katika mazoezi hayo, ambayo yanafanywa katika Bahari ya Pasifiki na Arctic, pamoja na zile za mataifa ya Baltic na Caspian.

Soma pia;Ukraine yaendelea kuyalenga maeneo ya Urusi

Wizara hiyo ya ulinzi imesema luteka hizo zitahusisha pia zaidi ya mazoezi 300 ya vita kwa kutumia kwa vitendo halisi silaha za vita.

Mazoezi yanalenga kupima utayari wa vitengo vya Urusi

Wizara yaulinzi ya Urusi imeongeza kwamba madhumuni makuu ya mazoezi hayo ni kupima vitendo vya kamandi ya jeshi la wanamaji katika ngazi zote, na pia utayari wa wafanyakazi wa melini, vitengo vya anga vya jeshi hilo la wanamaji na vikosi vya pwani.

Vikosi vya Urusi kufanya mazoezi katika maeneo yao ya kuhudumu

Vikosi kutoka vitengo vinne kati ya vitano vya jeshi la wanamaji la Urusi ambavyo ni vile vya Kaskazini, Pasifiki, Baltic, na Caspian Flotilla vitashiriki, kila moja kikifanya mazoezi ya mafunzo katika maeneo yanapoendesha shughuli zake.

Kitengo cha tano cha Urusi chapata hasara kubwa

Kikosi cha tano cha Urusi kilichoko katika Bahari Nyeusi, kinashiriki katika mashambulizi dhidi ya Ukraine, ambapo kimepata hasara kubwa katika zaidi ya miaka miwili ya mapigano.

Urusi yazima moto uliosababishwa na shambulizi la Ukraine

Urusi imesema leo kuwa imezima moto katika ghala la mafuta ambalo liliwaka moto kwa masaa 48 baada ya shambulizi la droni laUkraine.

Gavana wa Urusi katika eneo la mpaka kati ya Urusi na Ukraine la Kursk, Alexei Smirnov, amethibitisha hayo.

Kituo cha kuhifadhi mafuta katika eneo la Bryansk nchini Urusi chateketeaPicha: Yevgeny Shchukin/ITAR-TASS/IMAGO

Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, Smirnov ameongeza kuwa matangi matatu ya mafuta yalilengwa na droni hilo la Ukraine, saa za mapema siku ya Jumapili lakini hakuna aliyejeruhiwa.

Ukraine iko tayari kutatua masuala ya mafuta na Slovakia

Ukraine imesema iko tayari kutatua masuala ya usafirishaji wa mafuta na Slovakia kuambatana na utaratibu unaofaa katika makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya. Haya yameelezwa leo na naibu waziri wa nishati wa Ukraine Roman Andarak.

Soma pia:Zelensky asema wanajeshi wake wanakabiliwa na wakati mgumu katika uwanja wa mapambano

Katika taarifa, Andarak amesema kuwa upande wa Ukraine uko tayari kusuluhisha uwezekano wa masuala yenye utata katika ngazi ya kitaalamu ikiwa upande wa Slovakia utatumia utaratibu husika uliotolewa kwenye makubaliano hayo ya Umoja wa Ulaya ambao Slovakia haujaufuata kufikia sasa.

Slovakia yatoa masharti kwa Ukraine

Waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico, alisema nchi yake itasitisha usambazaji wa dizeli kueleka Ukraine ikiwa nchi hiyo haitaruhusu usambazaji wa mafuta ya kampuni ya Urusi ya Lukoil kupitia eneo hilo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW