1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaanza luteka za kijeshi kubwa zaidi kuwahi kutokea

Daniel Gakuba
11 Septemba 2018

Jeshi la Urusi limeanza luteka kabambe za kivita zinazoshirikisha wanajeshi karibu 300,000 na zana nyingi za kijeshi. Luteka hizo zinazofanyika Mashariki mwa nchi zinawashirikisha pia wanajeshi wa China na Mongolia.

2018 Internationale Armeespiele
Picha: Reuters/M. Shemetov

 

Luteka hizo zilizopachikwa jina la Vostok 2018, maana yake, Mashariki 2018, zinafanyika upande wa Mashariki mwa Urusi, zikifika katika Bahari ya Pasifiki na Bahari ya Kaskazini.

Akizungumzia ukubwa wa luteka hizo, Mkuu wa jopo la majenerali katika jeshi la Urusi Valery Gerasimov alisema zitawahusisha wanajeshi 297,000, ndege za kivita zipatazo 1000, helikopta, ndege zisizoendeshwa na rubani, vifaru na magari mengine ya kijeshi vipatavyo 36,000, na manowari 80.

Umoja wa Kujihami wa NATO unaozijumuisha nchi nyingi za Magharibi umezikosoa luteka hizo, ukisema unazichukulia kama matayarisho ya Urusi ya kushiriki katika vita kubwa. Lakini Naibu waziri wa Ulinzi wa Urusi Alexander Fomin amesema hofu hiyo ya NATO haina msingi.

''Nataka kusisitiza kwamba hakuna sehemu ya luteka za kijeshi za Urusi ambazo zinaelekezwa kuilenga Jumuiya ya NATO wala Umoja wa Ulaya hata chembe. Katika Luteka hizi, pande zinazojiweka katika nafasi ya adui hazitumii kamwe sare za NATO wala kuzungumza Kiingereza. Hii ni kinyume na NATO ambazo katika luteka zake upande unawekwa katika nafasi ya adui huvalia sare za kisovieti au za jeshi la Urusi, kutumia vifaa vilivyotengenezwa Urusi, na kuzungumza kirusi.'' Alisema waziri huyo.

Haki ya kujilinda isiyo na mbadala wake

Katika luteka hizo Urusi inazitumia zana zake mpya za kijeshi, zikiwemo ndege na vifaruPicha: Reuters/M. Shemetov

Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmirty Peskov alizizungumzia pia luteka hizo, akisema katika mazingira ya sasa ambayo sio ya kirafiki, uwezo wa Urusi kujilinda sio tu kwamba ni halali, bali pia ni muhimu na hakuna chaguo mbadala.

Luteka hizi zinaanzia katika mkoa wa Mashariki wa Siberia, na zitadumu kwa wiki nzima zikiwahusisha pia wanajeshi wa China wapatao 3000, na wengine kutoka Mongolia. Rais Vladimir Putin anatarajiwa kushuhudia luteka hizo, baada ya kuufungua mkutano wa kiuchumi katika mji wa Mashariki wa Vladivostok, ambako Rais Xi Jinping ni miongoni mwa wageni mashuhuri wanaoshiriki.

Mazoezi haya ya kivita yanafanyika wakati Urusi ikiwa katika mvutano mkubwa na nchi za Magharibi, ambazo zinaituhumu kuingilia katika masuala ya ndani ya nchi hizo, na kuhusika katika mizozo ya kivita nchini Syria na Ukraine.

Marudio ya enzi za Kisovieti

Jeshi la Urusi linayazilinganisha luteka hizi na nyingine kubwa zilizofanyika mwaka 1981, wakati huo chini ya utawala wa Kisovieti, ambazo zilijulikana kama Zapad-81, yaani Magharibi 81. Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema kuwa luteka za wakati huu ni kubwa zaidi. Waziri Shoigu amesema luteka hizi zitafanyika katika mazingira yanayokaribiana kabisa na ya vita halisi.

Urusi inatarajiwa kutumia silaha zake mpya na za kisasa, zikiwemo makombora ya Iskander yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia, itatumia pia vifaru chapa T-80 na T-90, hali kadhalika ndege zake mpya chapa Su-34 na Su-35 ambazo tayari inazitumia katika vita nchini Syria.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, ape

Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW