1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtiririko wa gesi kutoka Urusi kuelekea Ulaya waanza tena

21 Julai 2022

Urusi imeanza tena kusukuma gesi kuelekea Ulaya kupitia bomba lake kubwa zaidi la Nord Stream 1 na hivyo kupunguza hofu ya mataifa ya magharibi kuhusu ugavi wa nishati hiyo wakati wa kipindi cha baridi.

Deutschland | Nord Stream 1 in Lubmin
Picha: Sean Gallup/Getty Images

Usambazaji wa gesi kupitia bomba la Nord Stream 1, ambalo hupita chini ya Bahari ya Baltic kuelekea Ujerumani, ulisitishwa kwa ajili ya matengenezo mnamo Julai 11 lakini, hata kabla ya hapo, mtiririko wa gesi ulikuwa umepunguzwa hadi asilimia 40 ya uwezo wa bomba hilo kutokana na mzozo uliochochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Takwimu za uwezo wa Nord Stream zimeonyesha kuwa mtiririko wa leo Alhamisi umerejea katika kiwango cha uwezo huo wa asilimia 40. Hatua hii imepokelewa vyema na raia wa Ulaya kama anavyoeleza Jens Hofmeister, raia wa Ujerumani.

"Nimefarijika kwamba gesi inatiririka tena. Lakini pia nina imani kwamba sisi kama nchi hatupaswi kuruhusu kutishiwa na Urusi, na kwa hivyo nina hisia mseto. Nadhani tutapata suluhu kwa njia moja au nyengine. Ninapotazama mjadala wa sasa wa nishati mbadala ninapata matumaini kuwa tutashinda kama nchi."

Soma zaidi: Urusi imelifunga bomba la gesi inayoingia Ujerumani

Usitishwaji wa usambazaji wa gesi ulitatiza juhudi za mataifa ya Ulaya kujiwekea akiba ya kutosha ya gesi kwa ajili ya majira ya baridi, jambo linaloongeza hatari ya kutokea mgao wa nishati na kikwazo kwa ukuaji wa uchumi uliyo dhaifu ikiwa Moscow itachukua hatua zaidi ili kulipiza kisasi kwa vikwazo vya Magharibi juu ya vita nchini Ukraine.

Picha: Dmytro Smoliyenko/Avalon/Photoshot/picture alliance

Makubaliano ya usafirishaji wa nafaka

Jana Jumatano, Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Urusi inatumia nishati yake kama silaha, na kwamba Mataifa ya Ulaya yanapaswa kujiandaa kwa hali mbaya zaidi. Kremlin inasema Urusi ni muuzaji wa kuaminika wa nishati lakini inakemea vikwazo dhidi yake kwa kupunguza mtiririko wa gesi.

Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema leo kwamba ana "matumaini" kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa hivi karibuni ambayo yatazingatia wasiwasi wa Urusi na kuruhusu nafaka ya Ukraine kuvuka Bahari Nyeusi.

Soma zaidi: Urusi yataka UN kuingilia mazungumzo ya nafaka

Kauli hii inajiri siku moja baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kuweka sharti jipya ambalo halikutarajiwa la kuwa makubaliano yoyote yatashughulikia pia mauzo ya nafaka iliyozuiwa nchini mwake.

Hadi tani milioni 25 za ngano na nafaka nyingine zimezuiliwa katika bandari za Ukraine na meli za kivita za Urusi na mabomu ya majini yaliyotegwa na Kyiv ili kujilinda na shambulio la Urusi. Mgogoro huo umepelekea bei za vyakula kupanda duniani kote na kuwasukuma mamilioni ya watu katika nchi maskini zaidi duniani kwenye hatari ya baa la njaa.

(AFPE, RTRE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW