1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaanzisha "Kura ya Maoni" ili kutwaa mikoa ya Ukraine

23 Septemba 2022

Urusi imeanzisha leo kile inachokiita kura ya maoni katika maeneo inayoyakalia kimabavu mashariki na kusini mwa Ukraine ili kuamua kama mikoa hiyo itaunganishwa na Urusi.

Russland | Vorbereitungen für Scheinreferendum in Donezk Region
Picha: Yegor Aleyev/TASS/dpa/picture alliance

Mikoa minne tayari imetangaza kuanza kwa zoezi la upigaji kura itakayofanyika kuanzia leo hadi Jumanne wiki ijayo katika mikoa minne ya Luhansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhzhia, inayowakilisha karibu asilimia 15 ya ardhi ya Ukraine.

Mamia kwa maelfu ya watu wataweza kupiga kura hadi Septemba 27. Mkoa wa Luhansk umetangaza kuwa raia ambao wamekimbilia Urusi wataweza kupiga kura wakiwa huko.

Kiongozi wa wanaotaka kujitenga na Ukraine huko Donetsk Denis Pushilin ameizungumzia siku hii kama muhimu na ya kihistoria na kusema huu ndio uhalisia wa sasa.

Soma zaidi: Scholz autaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuwa ubeberu

Urusi inataka kutumia matokeo ya kura hiyo ya maoni ili kuyaunganisha maeneo hayo kwa kigezo cha "haki ya watu kujiamulia wenyewe". Ukraine na hata jumuiya ya kimataifa zimetaja kutoitambua kura hiyo wakati Urusi wakiikalia kimabavu ardhi ya Ukraine.

Raia akishiriki "kura hiyo ya maoni" huko ZaporizhzhiaPicha: RIA Novosti/Sputnik/SNA/IMAGO

Kura hiyo ya maoni si halali

Kura hiyo ya maoni haizingatiwi kama halali kwa sababu inafanyika bila ya ridhaa ya Ukraine, chini ya sheria ya kijeshi na si kwa mujibu wa kanuni za kidemokrasia. Lakini pia waangalizi wa kimataifa hawawezi kufanya kazi yao kwa uhuru. Matokeo yenye upendeleo kwa Urusi yanatarajiwa kuwa na athari kubwa.

Soma zaidi:Maoni: Putin hana budi kuchochea vita ili anusurike 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameishutumu kura hiyo ya maoni huku akiwapongeza washirika wa Magharibi kwa kulaani hatua za Urusi. Wananchi pia wa Ukraine wanaipinga kura hiyo kama anavyoeleza Tatiana ambaye ni mkimbizi wa ndani kutoka Kherson:

"Ninapinga kura ya maoni. Nadhani mji wetu na eneo letu ni mali ya Ukraine. Hii ni hali ngumu mno na ninafikiri hakuna nafasi ya Warusi katika ardhi yetu."

Kura hiyo inajiri baada ya Ukraine mwezi huu kuyakomboa tena kwa wingi maeneo yake baada ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza, ikiwa ni miezi saba tangu Urusi kuivamia na kuanzisha vita vilivyoua maelfu ya watu, na kupelekea mamilioni ya wengine kuyakimbia makazi yao na kuvuruga uchumi wa dunia.

Wiki hii Rais wa Urusi Vladimir Putin alitangaza rasimu ya jeshi ya kuwasajili wanajeshi wapya 300,000 ili kushiriki vita vya Ukraine, katika harakati za Moscow kujaribu tena kuudhibiti mzozo huu.

(DPAE, RTRE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW