1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yadai kuiteka Bakhmut, mwanablogu wake maarufu auwawa

3 Aprili 2023

Mwanablogu maarufu wa vita Urusi Vladen Tatarsky ameuwawa kwa bomu katika mgahawa mmoja mjini Saint Petersburg, katika kile kinachoonekana kama mauaji ya pili ndani ya Urusi, ya mtu anayehusika na vita vya Ukraine.

Russland Militärblogger Vladlen Tatarsky
Picha: Telegram @Vladlentatarskybooks/via REUTERS

Tatarsky ambaye jina lake kamili ni Maxim Fomin, alikuwa na zaidi ya wafuasi 560,000 katika mtandao wa kijamii wa Telegram na alikuwa mmoja wa wanablogu maarufu zaidi wa vita ambao wameviunga mkono vita nchini Ukraine na wakati mwengine kuukosoa uongozi wa jeshi la Urusi pia.

Shirika la habari la TASS nchini Urusi limemnukuu mtu mmoja ambaye hakutaka kutambulishwa akisema bomu hilo lilikuwa limetegwa katika sanamu aliyopewa Tatarsky kama zawadi wakati alipokuwa akizungumza na watu kadhaa katika mgahawa huo. Alipoichukua na kuiweka kando ndipo mlipuko huo ulipotokea. Watu 25 wamejeruhiwa huku 19 kati yao wakiwa wanatibiwa hospitali.

Mkahawa alimokuwa Tatarsky baada ya mlipukoPicha: Investigative Committee of Russia/Handout via REUTERS

Haikubainika wazi ni nani aliyehusika na shambulizi hilo ila kamati ya Uchunguzi ya Urusi imesema imeanzisha uchunguzi wa mauaji.

Ukraine yanyoshewa kidole cha lawama

Kifo cha Tatarsky kinafuatia kifo chake Darya Dugina ambaye bomu lilitegwa katika gari lake mnamo mwezi Agosti mwaka uliopita. Dugina alikuwa mchambuzi maarufu wa siasa za kizalendo. Idara ya usalama ya Urusi iliituhumu Ukraine kwa kufanya shambulizi hilo ambalo Rais Putin aliliita la "kishetani."

Afisa mmoja mwandamizi Urusi ameinyoshea Ukraine kidole cha lawama kwa shambulizi hilo la Jumapili bila kutoa ushahidi naye mshauri mmoja wa rais wa Ukraine amesema nchini Urusi kunaanza kile alichokiita, "ugaidi wa ndani" baada ya shambulizi hilo.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi haikumlaumu yeyote kwa shambulizi hilo ila ikasema, kimya kilichopigwa na mataifa ya Magharibi ni jambo linaloonyesha unafiki ukizingatia kuwa nchi hizo huwa mstari wa mbele kuhusiana na mambo yanayowahusu waandishi wa habari.

Hayo yakiarifiwa kundi la mamluki wa Urusi la Wagner Jumatatu kupitia mkuu wake Yevgeny Prigozhin limedai kuwa "kimsingi" limeshauteka mji wa Bakhmut ulioko mashariki mwa Ukraine huku majeshi yake sasa yakiwa yanadhibiti afisi za serikali ya mji huo.

Kiongozi wa kundi la Wagner Yevgeny PrigozhinPicha: Sergei Ilnitsky/Pool EPA via AP/dpa/picture alliance

Mji usio na thamani ya kimkakati

Lakini usiku wa kuamkia Jumatatu, Rais Volodymyr Zelenskiy amewasifu wanajeshi wa nchi yake wanaoendelea kuupigania mji huo.

"Hoja ya kwanza ni jeshi na nafikiri tutauchukua, namshukuru kila mmoja anayeupeleka wakati huu mbele, Niwashukuru wanajeshi wetu wanaopigana karibu na Avdiivka, Maryinka, Bakhmut na hasa Bakhmut, kunatokota huko leo," alisema Zelenskiy.

Mapambano ya kuiwania Bakhmut ndiyo mapigano ya Urusi yaliyodumu kwa muda mrefu nchini Ukraine. Urusi na Ukraine zimeekeza sana katika mapambano ya kuchukua udhibiti wa mji huo ingawa wachambuzi wanasema mji wenyewe una thamani ndogo ya kimkakati.

Ukraine kwa upande wake inasema mapambano ya mji huo wa viwanda ni muhimu kwa ajili ya kuyazuia majeshi ya Urusi katika eneo zima la mashariki.