1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi yadai kupata mafanikio kwenye uwanja wa vita

Hawa Bihoga
29 Julai 2024

Urusi imesema leo vikosi vyake vimeteka kijiji cha Vovche mashariki mwa Ukraine, ikiwa ni mafanikio ya karibuni zaidi katika mkururo wa mafanikio ya Moscow katika wiki za karibuni.

Ukraine | Wanajeshi wakipokea maagizo
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika uwanja wa vita wakipokea maelekezo.Picha: Ashley Chan/Sipa USA/picture alliance

Tangazo hilo limekuja wakati ambapo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akizuru vikosi maalumu katika mkoa wa mpakani wa Kharkiv, ambako majeshi ya Urusi yalifanya mashambulizi ya kustukiza ya ardhini mwezi Mei, lakini yameshindwa kupata mafanikio ya maana. 

Zikiwa katika mwaka wa tatu wa mapigano, siyo Kyiv wala Moscow iliyoweza kubadili mwelekeo wa vita hivyo katika upande wake, licha ya vikosi vya Moscow kupata mafanikio katika mapambano ya ardhini katika miezi ya karibuni.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema katika mkutano wake wa kila siku kuwa vikosi vyake vimekikomboa kijiji cha Vovche kilichopo katika mkoa wa mashariki ya Donetsk.

Soma pia:Shambulizi la Ukraine lateketeza kituo cha mafuta cha Urusi

Kijiji hicho kiko umbali wa kilomita 16 kaskazini-mashariki mwa Avdiivka, ambao ni mji wa viwanda uliotekwa na Urusi mnamo mwezi Februari.

Mamlaka za Ukraine ziliwahimiza wakaazi waliosalia kuondoka Vovche mwezi uliopita, katikati mwa mashambulizi ya anga ya Urusi, huku taarifa zikisema ni watu saba tu ndiyo waliobaki kijijini hapo katika wakazi jumla 100 waliokuwepo kabla ya vita.

Mkoa wa viwanda wa Donetsk umeshuhudia mapigano makali zaidi kati ya vikosi vya Ukraine na majeshi ya uvamizi ya Urusi na umedhibitiwa kwa sehemu na waasi wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi tangu mwaka 2014.

Urusi yadai kupata mafanikio zaidi Ukraine

Kremlin imedai kuutwa mkoa huo pamoja na mikoa mingine mitatu ya Ukraine mwishoni mwa 2022, licha ya kutoidhibiti kikamilifu.

Mkuu wa Ukraine wa mkoa wa Donetsk Vandy Filashkin alisema vikosi vya Urusi viliuwa watu watatu na kuwajeruhi wengine watatu leo Jumatatu katika mji wa Toretsk, ulioko chini ya udhibiti wa Ukraine.

Wanajeshi wa Ukraine katika uwanja wa vita eneo la DonetskPicha: Jose Colon/Anadolu/picture alliance

Vikosi vya Urusi vimekuwa vikiusogelea mji huo ambao ulikuwa nyumbani kwa karibu watu 30,000, katika mashambulizi mapya baada ya kupindi cha utulivu kiasi.

Mkoa wa Kharkiv ambao Rais Zelenskiy ameutembelea leo, umekuwa chini ya mashambulizi ya kila siku ya vikosi vya Urusi tangu vilipovamia mwezi Februari 2022.

Soma pia:Urusi yaionya Armenia dhidi ya usuhuba na Magharibi

Zelenkiy ameuelezea uwanja wa mapambano mkoani humo kuwa mmoja ya magumu zaidi na kuviambia vikosi vilivyoko huko kuwa nchi nzima inawategemea wao.

"Napenda kukushukuruni. Tafadhali chukuweni tahadhari." Aliwaambia wanajeshi ambao walishangilia katika kila neno ya hotuba yake.

Aliongeza kwamba "nafasi zenu ziko hapa, katika mwelekeo huu, na yumkini ndiyo maeneo yenye joto kali kwenye uwanja wa mapambano. Nchi nzima inawategemea nyinyi.Tutashinda vita hivi. Ushindi kwa Ukraine."

Ukraine: Tumezuia mashambulizi ya Urusi

Jeshi la Ukraine limesema leo limezuwia mashambulizi sita ya Urusi dhidi ya Kharkiv katika muda wa siku moja iliyopita, ikiwemo mji wa Vovchansk.

Vikosi vya Urusi vimekuwa vikijaribu kuuteka mji huo mdogo ulioko umbali wa kilomita tano kutoka mpaka wake tangu kuanza kwa mashambulizi dhidi ya Kharkiv mwezi Mei.

Soma pia:Zelensky asema wanajeshi wake wanakabiliwa na wakati mgumu katika uwanja wa mapambano

Katika taarifa nyingine, Ukraine imeutaka Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kuchunguza shambulio dhidi ya gereza katika mkoa wa Donetsk lililouwa wafungwa kadhaa miaka miwili iliyopita.

Shambulio hilo dhidi ya gereza la Olenivka, usiku wa Julai 29 miaka miwili iliyopita, liliuawa watu wasiopungua 50 na kuwajeruhi wengine wasiopungua 130 kwa mujibu wa serikali ya Ukraine.

Kwanini Umoja wa Mataifa unashindwa kumaliza mizozo duniani?

01:22

This browser does not support the video element.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW