1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yadai kuvunja mashambulizi makubwa ya Ukraine

5 Juni 2023

Maafisa wa Urusi wamesema vikosi vyake vimezuia mashambulizi makubwa ya Ukraine katika majimbo mawili yaliyotwaliwa kinyume cha sheria na Moscow.

Russland | Schäden durch Militärangriff auf Donezk
Picha: Valentin Sprinchak/dpa/TASS/picture alliance

Ukraine haijathibitisha mashambulizi hayo, jambo linalofanya ukweli wa madai ya Urusi usiaminike moja kwa moja au kama waliashiria mwanzo wa mashambulizi yaliyotarajiwa ya Ukraine.

Katika kanda nadra ya video ambayo ilitolewa asubuhi ya Jumatatu, wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema vikosi vyake vilirudisha nyuma mashambulizi makubwa ya Ukraine yaliyofanywa Jumapili katika maeneo matano kusini mwa jimbo la Donetsk.

Jimbo hilo ni kati ya majimbo manne ambayo rais wa Urusi Vladimir Putin husema ni sehemu ya nchi yake, hata ingawa sehemu yake tu ndiyo inadhibitiwa na Urusi.

Soma pia: Zelenskiy watoto wasiopungua 500 wameuwawa Ukraine

 Igor Konashenkov  ambaye ni msemaji wa wizara ya Ulinzi ya Urusi amesema lengo la adui lilikuwa kuvunja ngome zao katika maeneo yenye ulinzi mdogo kwenye uwanja wa mapambano. Lakini lengo lao halikufaulu.

 "Adui hakufanikiwa kwenye malengo yake. Kutokana na uwezo na majibu yaliyopigiwa hesabu na vikosi vya ‘Mashariki', jeshi la Ukraine lilipoteza zaidi ya wapiganaji 250, vifaru 16, zana za mizinga na magari maalum 21 ya kivita,” amesema Konashenkov.

Vladimir Rogov, gavana wa Urusi aliyewekwa kusimamia jimbo la kusini mashariki mwa Ukraine Zaporizhzhia, amesema vikosi vya Ukraine pia vilijaribu kuvunja ngome za Urusi, lakini vilitimuliwa baada ya kusogea mita 400 karibu na eneo linalokaliwa na Urusi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika mojawapo ya kanda za video akilihutubia taifa lake kuhusu hali ya vita nchini mwake.Picha: https://www.president.gov.ua

Soma pia: Kiev yashambuliwa tena na Urusi, Zelenskiy asafiri kwenda Moldova

Rogov amesema uhasama ulianza tena mapema Jumatatu, na kuongeza kuwa adui alituma kikosi kikubwa zaidi kuliko kilichofanya mashambulizi siku ya Jumapili.

Maafisa wa Ukraine hawakuthibitisha mashambulizi hayo. Kituo cha mawasiliano ya kimkakati ya vikosi vya majeshi ya Ukraine, kimesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba vikosi vya Urusi vinaimarisha shughuli zao za habari na saikolojia.

Soma pia: Ukraine yapuuzia mpango wa kumaliza vita kati yake na Urusi

Kupitia taarifa kituo hicho kimesema ili kuwavunja moyo Waukraine na kupotosha jamii, maafisa wa Urusi wanaoeneza propaganda watasambaza taarifa za kupotosha kuhusu mashambulizi makali ya Ukraine, wanakoelekea na hasara kwa Ukraine, hata kama hakuna mashambulizi.

Katika tukio jingine, kiongozi wa kampuni ya wapiganaji binafsi ya Urusi Wagner, Yevgeny Prigozhin, amesema leo Jumatatu kwamba vikosi vya Ukraine vimechukua udhibiti wa sehemu yake ya makaazi ya Berkhivka, kaskazini mwa Bakhmut, hali ambayo ameita kuwa "aibu”.

Mamluki wa Wagner walikamata Bakhmut mwezi uliopita baada ya mapambano ya muda mrefu, kisha walikabidhi ngome zao kwa vikosi vya kawaida vya Urusi.

(Vyanzo: APE, RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW