Urusi yadai kuwa wanajeshi wake wameukamata mji wa Soledar
13 Januari 2023Urusin imedai kuwa wanajeshi wake wameukamata mji wa uchimbaji chumvi unaogombaniwa vikali wa Soledar mashariki mwa Ukraine. Kama ni kweli, basi unaweza kuwa ni ushindi wa nadra wa Kremlin katika uvamizi wake wa Ukraine.
Maafisa wa Ukraine, hata hivyo, wamekanusha ripoti hizo wakisema mapigano bado yanaendelea mjini humo.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Luteni Jenerali Igor Konashenkov amesema ukombozi wa mji wa Soledar ulikamilika usiku wa Januari 12 akiongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu kazika muendelezo wa harakati za mashambulizi katika mkoa wa Donetsk.
Amesema kuukamata mji huo kutawawezesha wanajeshi wa Urusi kukata barabara za kusambaza vifaa kwa wanajeshi wa Ukraine katika mji wa Bakhmut na kisha kuvizingira vikosi vwa Ukraine katika eneo hilo. Soledar inapatikana katika mkoa wa Donetsk, mmoja kati ya minne ambayo Moscow iliikwapua Septemba mwaka jana.