1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yadai kuzima mashambulizi mengine ya Ukraine

6 Juni 2023

Urusi imesema kuwa imezima mashambulizi mengine makubwa ya vikosi vya Ukraine huko Donetsk, huku Kiev wakinadi kupiga hatua katika operesheni yao huko Bakhmut.

Ukraine I Kämpfe um Bakhmut
Picha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Taarifa hiyo ya Urusi imetolewa na Wizara ya Ulinzi iliyosema kuwa mbali na kuzima mashambulizi hayo ya Ukraine, wamesababisha pia hasara kubwa kwa majeshi ya Kiev na kuharibu vifaru vinane vya kivita chapa Leopard. Jana Jumatatu, Urusi ilisema kuwa Ukraine imeanzisha mashambulizi makubwa katika mkoa huo wa kusini.

Maafisa wa Ukraine wamethibitisha kuanza mashambulizi makubwa  katika baadhi ya maeneo na kusema kuna mafanikio yanayodhihirika huko Bakhmut. Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Ganna Malyar amesema Urusi imekuwa ikitoa taarifa hizo mara kwa mara ili kuficha ukweli kwamba wamekuwa wakishindwa mapambano huko Bakhmut.

Licha ya Urusi kudai kuyazima mashambulizi hayo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewapongeza wanajeshi wake kwa hatua waliyofikia huko Bakhmut:

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: president.gov.ua

" Ninatoa shukrani zangu kwa kila askari wetu, kwa watetezi wetu wote, ambao wametupa habari tuliyokuwa tunaisubiri leo. Mumefanya kazi nzuri kuelekea huko Bakhmut, hongereni askari! Tunaona jinsi Urusi inavyobabaika kwa kila hatua tunayopiga huko, kwa kila sehemu tunayochukua. Adui anajua wazi kuwa Ukraine itashinda. Wanashuhudia na kuhisi hilo kutokana na mashambulizi yenu, hasa katika mkoa wa Donetsk. Asanteni kwa hilo!"

Soma pia: Mashambulizi nchini Urusi yaharibu dhana ya 'jeshi la Putin'

Urusi na Ukraine zimekuwa zikidai kusababisha hasara kubwa kwa upande mwingine, taarifa ambazo mara kadhaa zimekua vigumu kuthibitishwa. Hata hivyo, Mkuu wa kundi la mamluki la Urusi la Wagner, Yevgeny Prigozhin, amesema jana kuwa wanajeshi wa Ukraine wamepata mafanikio karibu na mji huo wa Bakhmut.

Madai hayo tofauti yanajiri wakati mjumbe wa amani wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, Kadinali Matteo Zuppi, amewasili mjini Kyiv kwa mazungumzo ya siku mbili. Jana, Rais wa Marekani Joe Biden amesema anaitakia mema Ukraine katika mashambulizi yake makubwa yaliyokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu.

Kesi katika Mahakama ya ICJ kusikilizwa

Jengo la Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) The Hague, UholanziPicha: Yves Herman/REUTERS

Wakati hayo yakiarifiwa, leo hii Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) yenye makao yake mjini Hague, Uholanzi itasikiliza kesi iliyoanzishwa na Ukraine mwaka 2017 kufuatia uchokozi wa Urusi mashariki mwa Ukraine, hata kabla ya kuanza kwa uvamizi huu wa sasa.

Soma pia: Urusi yadai kuvunja mashambulizi makubwa ya Ukraine

Urusi inakabiliwa na mashitaka inayoyakanusha ya kuwasaidia waasi wanaoiunga mkono Moscow katika eneo la Donbass kwa kuwapatia silaha na fedha na hivyo kukiuka Mkataba wa Kimataifa dhidi ya ufadhili wa Ugaidi. Urusi pia inashtumiwa kuwakandamiza watu wasio na asili ya Urusi huko Crimea.

Katika kesi hiyo, wawakilishi wa Ukraine watasikilizwa na Mahakama hiyo leo hii huku wale wa Urusi wakipanda kizimbani siku ya Alhamisi. Hadi sasa haijulikani ni lini hukumu ya mwisho ya Mahakama hiyo ya ICJ itatolewa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW