1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendelea kufanya mashambulizi nchini Ukraine

27 Oktoba 2022

Mashambulizi ya anga ya Urusi yamehujumu maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv katika wakati Moscow imetishia pia kwamba inaweza kuilenga miundombinu ya mawasiliano ya Marekani iwapo itatumika katika vita.

Ukraine Krieg Hunde
Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Kwa mujibu wa gavana wa eneo moja la mji mkuu wa Ukraine Kyiv, Olexiy Kuleba  makombora ya ndege za Urusi yameilenga wilaya moja ya mji mkuu mapema leo Alhamisi.

Akiandika kupitia mtandao wa Telegram Kuleba hakuutaja mji ulioshambuliwa lakini amesema vikosi vya uokozi vilitumwa kwenda kutoa msaada wa dharura kwenye eneo hilo. Katika ujumbe wake afisa huyo amesema baadhi ya makombora yalidunguliwa na mifumo ya ulinzi ya Ukraine.

Mashambulizi hayo mapya yametokea saa chache baada ya ving´ora vya tahadhari kwenye mji mkuu kyiv kusikika mara nne hapo siku ya Jumatano.

Picha: Konstantin Mihalchevskiy/SNA/IMAGO

Kwa kawaida ving´ora hivyo huwa ni ishara ya kukaribia kutokea mashambulizi na wakaazi wa mji huo hutakiwa kwenda maeneo salama ikiwemo mahandaki pindi vinaposikika.

Mbali ya mji mkuu, vikosi vya Urusi vimeyalenga pia maeneo kadhaa ya kusini mwa Ukraine vikitumia ndege 20 zisizo na rubani chapa Shahed-136 ambazo zinaaminika hutengenezwa nchini Iran.

Jeshi la Ukraine limesema hujuma hiyo ilitokea saa chache kabla ya usiku wa manane kuamkia leo. Hata hivyo inaarifiwa ndege 19 kati ya 20 zilidunguliwa na jeshi la Ukraine nyingi ikiwa ni jirani ya mkoa wa Odessa.

Hata hivyo taarifa nyingi kuhusu matukio kwenye uwanja wa vita haziwezi kuthibitishwa kutokana na mapigano yanayoendelea.

Kituo cha umeme huko rais ya Crimea chashambuliwa

Katika mkasa mwingine rasi ya Crimea ambayo ilinyakuliwa na Urusi kutoka Ukraine mnamo mwaka 2014 ni eneo jingine lililolengwa katika muda wa saa 24 zilizopita.

Gavana wa eneo hilo aliyeteuliwa na Moscow Mikhail Razvozhaev, amesema kituo kimoja cha kufua umeme huko Crimea kimeshambuliwa kwa ndege isiyo na rubani usiku wa kuamkia leo.

Shambulizi hizo kwenye mji mkuu wa Crimea, Sevastopol lilisababisha moto lakini hapajatokea madhara mengine makubwa. Huo ni mwendelezo wa kila upande kuilenga miundombinu muhimu hususani ya nishati kwenye uwanja wa vita.

Ukraine ambayo katika wiki za karibuni imepata pigo kutokana na kuharibiwa kwa vituo vingi vya kufua na kusambaza umeme bado inahangaika kuifanyia ukarabati miundombinu yake.

Zelensky awashukuru wafanyakazi wanaokarabati miundombinu ya umeme

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine Picha: Ukrainian President'S Office/APA Images/ZUMA/picture alliance

Katika hotuba yake ya kila siku kwa taifa, rais Volodmyr Zelenksy amewashukuru wafanyakazi wanaopambana kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana nchini humo licha ya hujuma zinazofanywa na jeshi la Urusi.

"Magaidi wa Urusi wametengeneza mazingira magumu sana kwa wafanyakazi wetu wa sekta ya nishati ambayo hayajawahi kushuhudiwa na yeyote barani Ulaya. Hapakuwahi kuwa na vitisho kama ambavyo wataalamu wetu wanalazimika kupambana navyo hivi sasa. Na wanakabiliana navyo kwa fahari" amesema Zelensky.

Katika hatua nyingine afisa mmoja wa Urusi amesema satelaiti za kampuni za Marekani na washirika wake huenda zitalengwa na Urusi iwapo zitatumika katika vita nchini Ukraine.

Afisa huyo wa wizara ya mambo ya kigeni mjini Moscow amesema Urusi itajibu iwapo miundombinu hiyo ya mawasiliano itatumika katika mzozo unaoendelea.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW