Urusi yaendelea kushambulia maeneo kadhaa nchini Ukraine
28 Januari 2026
Katika usiku wa kuamkia leo Jumatano Urusi imeishambulia Ukraine kwa ndege zisizo na rubani na makombora katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, huku mji wa kusini wa Odesa ukishambuliwa kwa usiku wa pili mfululizo, kwa mujibu wa taarifa ya leo ya maafisa wa Ukraine.
Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi iliushambulia mji mkuu Kiyv kwa kombora la Iskander-M pamoja na ndege zisizo na rubani 146 ambapo 103 kati ya hizo zimeharibiwa na ulinzi wa anga wa Ukraine.
Mashambulizi hayo mapya ya usiku wa kuamkia leo yametokea saa chache baada ya mashambulizi ya siku ya Jumanne usiku ambapo watu wasiopungua 12 walikufa kwenye sehemu mbalimbali nchini Ukraine, wakiwemo abiria watano katika treni iliyolengwa na ndege zisizo na rubani za Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema mashambulio hayo yanadhoofisha juhudi za amani na amewataka washirika waongeze shinikizo dhidi ya Urusi ili ivimalize vita dhidi ya nchi yake.
Mykola Kalashnyk, mkuu wa utawala wa kijeshi wa eneo la Kyiv, amesema watu wawili mume na mke wake walifariki kutokana na shambulio hilo na mtoto wao mwenye umri wa miaka minne na watu wengine watatu wamejeruhiwa.
Taarifa ya kikosi cha huduma za dharura imesema katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, jengo la makazi la ghorofa 17 lilishambuliwa.
Katika eneo la kati la Dnipropetrovsk, mashambulio ya ndege zisizo na rubani yamesababisha kifo cha mwanamume mmmoja aliyekuwa na umri wa miaka 46 na watu watano wamejeruhiwa mmoja wao vibaya sana.
Mji wa kusini mwa Ukraine, Odesa umeshambuliwa kwa siku mbili mfululizo, gavana wa kikanda amesema miundombinu inayozunguka maeneo ya bandari za Ukraine katika Bahari Nyeusi imeharibiwa.
Mashambulizi hayo mabaya yanayoendelea yamewaacha Waukraine wengi bila umeme katika kipindi hiki cha baridi kali tangu wapatanishi wa Urusi na Ukraine walipokutana katika Falme za Kiarabu wiki iliyopita kwa mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani yanayolenga kuumaliza mzozo kati ya Urusi na Ukraine.
Duru inayofuata inatarajiwa kufanyika Februari mosi, kulingana na Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky.
Wakati huo huo Zelensky aliyefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Stammer, amesema Ukraine inataka kukomesha vita haraka iwezekanavyo na iko tayari kufanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya amani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha, amesema Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky yuko tayari kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin, kujadili masuala nyeti kama sehemu ya juhudi za kuvikomesha vita.