1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendelea kuushambulia mji wa Mariupol nchini Ukraine

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
13 Aprili 2022

Mashambulizi hayo yaliendelea usiku kucha kuamkia siku ya Jumatano na maeneo yaliyolengwa zaidi ni bandari ya jiji hilo la Mariupol na eneo la Azovstal ambapo askari wa Ukraine wanalitumia kujihifadhi.

Angriff auf die Ukraine I Mariupol
Picha: Leon Klein/AA/picture alliance

Naibu meya wa mji wa Mariupol, Serhiy Orlov ameliambia shirika la habari la Ujerumani (ARD) kwamba wakazi wa mji huo wamezingirwa kwa muda wa wiki nzima na wakati wote huo wameteseka bila ya kuwa na maji, chakula au nguvu za umeme huku wengi wakijificha katika sehemu za chini ya nyumba zao kuepuka mashambulizi.

Uharibifu wa majengo katika mji wa Mariupol kutokana na vita vinavyoikumba Ukraine.Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Utawala wa mkoa wa Donetsk, ambako Mariupol ni mji mmoja wapo katika mkoa huo unakadiria kuwa zaidi ya watu 20,000 wameuawa. Kulingana na vyanzo vya Ukraine mashambulizi hayo yanayofanywa na wanajeshi wa Urusi yamefika hadi kwenye mji wa mashariki wa Kharkiv na yanatarajiwa kuendelea katika eneo la mashariki mwa Ukraine.

Wakati huo huo wizara ya ulinzi ya Urusi imesema zaidi ya wanajeshi elfu moja wa Ukraine wamejisalimisha katika mji wa Mariupol, mji wa kimkakati wa bandari ulioko mashariki mwa Ukraine ambao umezingirwa na wanajeshi wa Urusi kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Soma:Biden amtuhumu Putin kwa mauaji ya halaiki nchini Ukraine

Msemaji wa wizara hiyo amefahamisha kuwa wanajeshi wa Ukraine 1,026 wa kikosi cha 36 cha wanamaji wamejisalimisha na kuweka chini silaha zao kwa hiari. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema askari hao walijisalimisha karibu na kiwanda kikubwa cha chuma cha mjini Mariupol kinachoiwa Illich na miongoni mwao walikuwemo maafisa wa juu 162, kati yao 47 ni wanawake. Amesema zaidi ya askari 100 walijeruhiwa.

Amesema wanajeshi 151 wa Ukraine wa kikosi hicho cha 36 cha wanamaji waliojeruhiwa walipewa huduma ya kwanza mahala walipokuwa, na kisha wote wakapelekwa katika hospitali ya jiji la Mariupol kwa ajili ya kupata matibabu. Hata hivyo msemaji wa wizara ya ulinzi ya Ukraine amesema hana taarifa zozote juu ya kujisalimisha wanajeshi hao wa kikosi cha wanamaji cha Ukraine katika mji wa Mariupol.

Marais wa Poland Andrzej Duda, Gitanas Nauseda wa Lithuania, Egils Levits wa Latvia na Alar Karis wa Estonia waelekea mjini Kyiv kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.Picha: Office of the President of the Republic of Lithuania/REUTERS

Kwingineko marais wa Poland Andrzej Duda, Gitanas Nauseda wa Lithuania, Egils Levits wa Latvia na Alar Karis wa Estonia wanaelekea mjini Kyiv kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky. Viongozi hao wamesema ziara hiyo ni kwa ajili ya kuonyesha kuwa wanawaunga mkono Waukraine. Urusi iliivamia Ukraine mnamo Februari 24 katika hatua ambayo Moscow inaelezea kuwa ni operesheni maalum ya kijeshi dhidi ya jirani yake huyo wa upande wa kusini.

Vyanzo: DPA/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW