1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendeleza mashambulizi dhidi ya Ukraine

Sylvia Mwehozi
11 Agosti 2022

Ukraine imeishutumu Urusi kwa mashambulizi ya roketi yaliyosabbaisha vifo vya raia 14 karibu na kinu cha nyuklia, wakati kundi la nchi za G7 likionya kwamba udhibiti wa Moscow wa mtambo unahatarisha eneo zima.

Ukraine Krieg | Angriff auf Marhanez
Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Mashambulizi ya usiku kucha katika viunga vya katikati mwa Ukraine yamesababisha vifo vya watu 13 na wengine11 wamejeruhiwa, huku wengine watano wakitajwa kuwa katika hali mbaya.  Gavana wa mkoa wa Zaporizhzhia Oleksandr Starukh alisema raia mwingine mwanamke amepoteza maisha baada ya makombora ya Urusi kutua katika kijiji kimoja kwenye mkoa huo.

Ukraine na Urusi zimetupiana lawama kwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhiaambacho ni kikubwa barani Ulaya. Ukraine inadai kuwa Urusi imeweka mamia ya askari na kuiba silaha katika kinu hicho tangu ilipokidhibiti Machi 4, muda mchache baada ya uvamizi wake. Kinu hicho kimeshambuliwa mara kadhaa na kiliharibiwa kwa sehemu wiki iliyopita, walakini miundombinu muhimu imeelezwa bado inafanya kazi.

Mashambulizi hayo yametokea siku chache baada ya mlipuko mkubwa kutikisa kambi ya kijeshi ya anga ya Saki katika rasi ya Crimea iliyotwaliwa na Urusi. Mashambulizi hayo yamefufua kumbukumbu ya maafa ya nyuklia ya Chernobyl mnamo mwaka 1986 wakati wa enzi ya Kisovieti, yaliyowaua mamia ya watu na kusambaza uchafuzi wa mionzi katika sehemu kubwa ya Ulaya.

Wakati Moscow na Kiev zikiendelea kutupiana lawala juu ya mashambulizi, mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la nchi saba zilizopiga hatua kiviwanda ulimwenguni za G7 wameitaka Moscow kurejesha haraka udhibiti wa kinu cha nyuklia cha mikononi mwa Ukraine wakati hofu ya maafa ikizidi kuongezeka.

Mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia Picha: Dmytro Smolyenko/Ukrinform/IMAGO

Taarifa iliyotolewa na kundi la nchi za G7 imesema kuwa "wafanyakazi wa Ukraine wanaohusika na uendeshaji wa mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhya wanapaswa kuendelea na majukumu yao bila vitisho au shinikizo". Taarifa hiyo imeongeza kuwa hatua ya Urusi kuendelea kudhibiti kinu hicho inahatarisha eneo zima.

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa G7 wamesisitiza "umuhimu wa kuruhusu wataalamu wa shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za nyuklia, IAEA, kutumwa kwenye kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhya ili kushughulikia masuala ya usalama."

Wakati huohuo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura hii leo ili kushughulikia mzozo wa mashambulizi dhidi ya kinu hicho cha nyuklia nchini Ukraine. Duru za kidiplomasia katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York zimesema mataifa 15 wanachama wa baraza hilo yatajadili suala hilo, kufuatia ombi la Urusi, mojawapo ya wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama, pamoja na Uingereza, China, Ufaransa na Marekani ambao wana mamlaka ya kura ya turufu juu ya maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Hayo yakijiri, Umoja wa Mataifa umesema kuwa shehena ya kwanza ya ngano kutoka Ukraine inaweza kuondoka wiki ijayo chini ya makubaliano ya kihistoria ambayo yalisainiwa pia na Urusi yanayolenga kushughulikia mgogoro wa chakula duniani. Mratibu wa muda wa Umoja wa Mataifa katika kituo cha pamoja cha uratibu mjini Istanbul Frederick Kenney, amesema meli 12 za kwanza kuondoka bandari za Ukraine chini ya makubaliano hayo, zilikuwa zimebeba tani 370,000 za mahindi na bidhaa nyingine za chakula. Shehena ya kwanza ya nafaka iliyosafirishwa kwa meli iliyokuwa na bendera ya Sierra Leone, iliondoka katika bandari ya Odessa ya Ukraine mnamo Agosti 1 na ilitarajiwa kutia nanga katika bandari ya Tripoli ya Lebanon mwishoni mwa juma.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW