Urusi yazidi kulenga miundombinu Ukraine
31 Oktoba 2022Milipuko mikubwa imesikika kote katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv mapema asubuhi, wakati wakaazi wakijiandaa kwenda kazini.
Baadhi yao walipokea ujumbe mfupi wa simu kutoka idara ya matukio ya dharura kuhusu kitisho cha mashambulizi ya makombora, huku ving'ora vikilia kwa saa tatu mfululizo.
Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amesema maeneo makubwa ya mji huo yamekatiwa umeme na maji kutokana na mashambulizi hayo, na kuongeza kuwa maafisa wa jiji wlaikuwa wanafanya kazi kurekebisha kituo cha nishati kilichoharibiwa, ambacho kinasambaza umeme kwa makaazi 350,000 katika mji mkuu.
Soma pia: Rais wa Ujerumani asema taifa linakabiliwa na nyakati ngumu
Katika mji wa Kharkiv, mashambulizi mawili yamepiga miundombinu muhimu na njia ya chini ya ardhi iliacha kufanya kazi. Maafisa wameonya pia kuhusu uwezekano wa kukatika kwa umeme katika mji wa Zaporizhzhia kutokana na mashambulizi mjini humo.
Miundombinu muhimu pia imelengwa katika mkoa wa Cherkasy kusini-mashariki mwa Kyiv, na milipuko imeripotiwa katika mikoa mingine ya Ukraine. Katika mkoa wa Kirovohrad ulioko katikati mwa Ukraine, kituo cha nishati kilishambuliwa kulingana na mamlaka za mkoa huo.
Kisasi kwa mashambulizi dhidi ya meli zake bahari Nyeusi
Mashambulizi hayo yamekuja siku mbili baada ya kushtumu Ukraine kufanya shambulizi la droni dhidi ya meli zake katika bahari Nyeusi nje ya pwani ya rasi iliyonyakuliwa ya Crimea.
Soma pia: Putin asema hajutii kuivamia Ukraine
Ukraine imekana shambulizi hilo, na kusema Urusi ilishughulikia vibaya silaha zake, lakini bado Moscow ilitangaza kusitisha ushiriki wake katika makubaliano yalioongozwa na Umoja wa Mataifa kuruhusu njia salaama kwa meli zinazobeba nafaka kutoka Ukraine.
Kwenye ujumbe wake wa video kwa raia Ukraine katika siku ya 249 ya uvamizi wa Urusi, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameishtumu Urusi kutaka kuchochea mzozo wa chakula duniani kwa hatua yake na kuongeza kuwa hilo linadhihirisha kuwa Moscow siyo mshirika wa kuaminika kwa ajili ya majadiliano.
"Ni nini dunia imesikia? Madai kwamba mtu amefyatua droni kutokea kwenye meli ya nafaka... Awali walizungumzia "ndege wa vita", kisha, "wadudu wa vita", na sasa, nafaka ya vita.. Ngano ya mauaji, inayowazamisha maafisa wa jeshi la wanamaji wa Urusi," alisema Zelenskiy.
Soma pia: Urusi yaendelea kufanya mashambulizi nchini Ukraine
"Nini unaweza kusema? Ni watu wagonjwa kabisa. Lakini watu hao wagonjwa wanairejesha tena dunia kwenye kingo za mzozo wa chakula, aliongeza Zelenskiy."
Uturuki kuendelea na juhudi za usafirishaji nafaka
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema nchi yake itaendeleza juhudi za usafirishaji wa nafaka licha ya kujitoa kwa Urusi, ili kuendelea kuhudumia wanadamu.
Katika tukio tofauti, msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema timu ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa na Uturuki ilikuwa imekamilisha ukaguzi wa meli ya kwanza kati ya 40 zilizopangwa kukaguliwa hii leo katika eneo la bahari la istanbul.
Awali ukaguzi huo ulikuwa unajumlisha wanachama kutoka Urusi na Ukraine, kabla ya kujitoa kwa Moscow.