1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendeleza mashambulizi ya makombora mkoa wa Donetsk

Sylvia Mwehozi
15 Agosti 2022

Vikosi vya Ukraine vimeripoti mashambulizi mazito ya makombora ya Urusi, inayojaribu kusonga mbele kwenye miji kadhaa katika mkoa wa mashariki wa Donetsk ambao umekuwa kitovu cha mashambulizi.

Ukraine Nikopol | Zerstörte Gebäude
Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Mkuu wa utumishi wa vikosi vya Ukraine pia ameripoti mashambulizi ya makombora kwenye miji zaidi ya dazeni katika eneo la mashariki hususan mkoa wa Kherson ambao unadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na wanajeshi wa Urusi, lakini ambako pia vikosi vya Ukraine vinadhibiti kwa kasi baadhi ya maeneo. Umakini umeelekezwa katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine katikati mwa wasiwasi wa kutokea maafa kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni ambayo Moscow na Kyiv zote zinatupiana lawama.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa rai ya kuanzishwa ukanda usio wa vita huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, akionya kwamba askari wa Urusi watakaokishambulia kinu hicho kikubwa barani Ulaya au kukitumia kama ngome ya mapigano, watalengwa na vikosi vya nchi yake.Urusi yakataa kurudishia Ukraine udhibiti wa kinu, nyuklia

"Wavamizi wanajaribu kuwatisha watu kwa njia ya kejeli sana, kwa kutumia mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia ZNPP. Wanajificha nyuma ya kituo kuishambulia Nikopol na Marganets. Wanafanya uchochezi wa mara kwa mara kwa kupiga makombora eneo la ZNPP na kujaribu kuongeza idadi ya wanajeshi huko ili kuendelea kuihujumu nchi yetu na ulimwengu mzima ulio huru," alisema Zelensky.

Sehemu ya mtambo wa nyukilia wa Zaporizhzhia Picha: ALEXANDER ERMOCHENKO/REUTERS

Kinu hicho kinatawala hifadhi kubwa ya ukingo wa mto Dnipro. Vikosi vya Ukraine vinavyodhibiti miji katika ukingo wa upande wa pili wa mto, vimeshuhudia mashambulizi makali kutoka kwa Urusi. Rais Zelensky amesema pia kuwa Ukraine mara kadhaa imependekeza mfumo tofauti kwa utawala wa Urusi juu ya mazungumzo ya amani bila ya mafanikio.

Wakati mashambulizi hayo yakiripotiwa, kwingineko meli zaidi zilizobeba nafaka ya Ukraine zinajiandaa kuondoka kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita ya kupunguza mzozo wa chakula duniani. Meli inayoelekea Ethiopia ambayo ni ya kwanza tangu uvamizi wa Urusi, ilikuwa inajiandaa kuondoka ndani ya siku chache zijazo, wakati duru nyingine zikisema meli ya kwanza iliyobeba nafaka iliyoondoka Ukraine inakaribia kufika Syria.

Hayo yakijiri, rais wa Urusi Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini wanatazamiwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia. Vyombo vya habari vya taifa vya Korea Kaskazini vimeripoti kwamba, Putin amemtumia salamu Kim hii leo wakati Pyongyang ikiadhimisha siku ya ukombozi kutoka utawala wa kikoloni wa Japan, na kusema kuwa nchi hizo mbili zinakusudua kupanua uhusiano, ambao pia utasaidia "kuimarisha usalama na utulivu kwenye Rasi ya Korea na katika eneo lote la Kaskazini-mashariki mwa Asia”.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW