1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yaendeleza mashambulizi yake nchini Ukraine

Zainab Aziz AFP/RTRE
30 Januari 2026

Urusi imeishanbulia Ukraine kwa kombora na zaidi ya droni 100. Wakati huo huo Zelensky amesema anatarajia juhudi za Marekani zitaifanya Urusi isimamishe mashambulizi yake kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine.

Vita vya Urusi nchini Ukraine | Kiyv
Jengo la maduka lililoharibiwa na vita vya Urusi katika jiji la Kiyv nchini UkrainePicha: Alex Chan Tsz Yuk/SOPA/ZUMA Press/picture alliance

Jeshi la anga la Ukraine limesema usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Urusi imeishambulia nchi hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kwamba Urusi imekubali kusitisha mashambulizi yake katika mji mkuu, Kiyv na pia katika miji mingine ya Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymir ZelenskyPicha: Ukrainian Presidential Office/AFP

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema anaishukuru Marekani kwa juhudi zake zinazolenga kuifanya Urusi isimamishe mashambulizi yake dhidi ya Ukraine na kwamba anaitegemea Marekani kuhakikisha kwamba Urusi inatekeleza ahadi yake ya kusitisha mashambulizi yake hasa kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine.

Akizungumza katika hotuba yake kwa njia ya video, Zelenskiy amesema hali ni ngumu zaidi katika mji mkuu wa Ukraine, Kiyv hasa kutokana na matatizo ya ukosefu wa umeme, Ameongeza kusema kwamba zaidi ya majengo 450 ya makazi katika wilaya kadhaa za jiji la Kyiv vifaa vyake vya kutia joto havifanyi kazi kutokana na mashambulizi ya Urusi yanayolenga miundombinu ya nishati.

Mashambulizi ya Urusi kwenye miundombinu ya umeme ya Ukraine katika siku za hivi karibuni yamesababisha mamilioni ya wakazi wa Ukraine kukosa joto majumbani mwao katika kipindi hiki cha baridi kali.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema siku ya Alhamisi kwamba yeye binafsi alimwomba Rais wa Urusi Vladimir Putin kusimamisha mashambulio hayo angalau kwa wiki moja kutokana na baridi kali inayowakumba watu wa Ukraine.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Joe Raedle/AFP/Getty Images

Wakati huo huo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, ameeleza kuwa tarehe au sehemu ya kufanyika mazungumzo  yanayosimamiwa na Marekani kati ya nchi yake na Urusi kuhusu kuvikomesha vita inaweza kubadilika. Duru inayofuata ya mazungumzo hayo ilikuwa ifanyike mjini Abu Dhabi siku ya Jumapili.

Kuhusu zoezi la kubadilishana wafungwa wa kivita kati ya Urusi na Ukraine Zelensky amesema Urusi imesimamisha zoezi hilo. Zoezi kama hilo lilifanyika mara ya mwisho mnamo mwezi Oktoba mwaka jana.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW