1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yafanya kura ya maoni ya kubadilisha katiba

25 Juni 2020

Mchakato wa kupiga kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba yanayoweza kumbakisha madarakati rais Vladmir Putin hadi mwaka 2036, umefunguliwa.

Russland Wladimir Putin hält eine Rede auf dem Roten Platz
Picha: Getty Images/Host Photo Agency/S. Guneev

Mchakato huo wa kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba ulipendekezwa na rais Vladmir Putin na awali ulipangiwa kufanyika Aprili 22 lakini kutokana na kuzuka kwa janga la virusi vya Corona ukaakhirishwa. Baade iliamuliwa mchakato huo uanze Julai mosi ambapo vituo vya kupiga kura vilitakiwa kuanza kufunguliwa wiki moja kabla ya hiyo Julai 1 ambayo ndiyo ya siku ya kilele ya mchakato huo. Lengo la vituo kufunguliwa wiki moja kabla ya hiyo Julai mosi ni kuepusha mikusanyiko mikubwa katika siku hiyo ya kilele.

Nini hasa kinachopendekezwa katoka mabadiliko hayo. Kimsingi mabadiliko ya katiba yanayopendekezwa ni pamoja na kutowa fursa ya kumruhusu rais Putin mwenye umri wa miaka 67 aliyeitawala Urusi kwa zaidi ya miongo miwili, kama rais au wazirti mkuu, kugombea kwa mara nyingine mihula miwili ya miaka 6 zaidi baada ya muhula wake huu utakapomalizika mwaka 2024.

Putin asema Warusi wengi wanamuunga mkono kubadilisha katiba

Mabadiliko mengine yanagusiana masuala ya kuboreshwa mafao ya kijamii, ufafanuzi wa ndoa kama muunganisho wa mume na mke pamoja na suala la kugawanywa kwa madaraka ya juu ya kiutendai ndani ya serikali kuimarisha nafasi ya rais.

Lakini ifahamike kwamba mageuzi haya ya katiba tayari yameshaidhinishwa na mabunge yote ya nchi hiyo, sambamba na mahakama ya katiba na kutiwa saini nna rais Putin. Rais huyo wa Urusi akasisitiza kwamba mageuzi hayo yaingie kwenye mchakato wa kupigiwa kura na wananchi licha ya kwamba haihitajiki kisheria. Wengi wanaiona hatua hii kama juhudi za kuiweka demokrasia katika mageuzi yenye utata.

Umaarufu wa Putin umeporomoka kutokana na COVID-19 nchini

Wapiga kura wakishiriki kura ya maoni kufanyia katiba ya Urusi mabadilikoPicha: DW/E. Barysheva

Juu ya hili hatua nzima ya kuufanya mchakato huu wa kura katikati ya janga la mripuko wa virusi vya Corona umezusha wasiwasi wa kiafya miongoni mwa jamii ya Warusi hasa ikizingatiwa nchi hiyo bado inaripoti visa zaidi ya 7000 vya maambukizi mapya kila siku na tayari watu 606,000 wamethibitika kuwa na maambukizi na kuifanya nchi hiyo kuwa ya tatu duniani yenye visa vingi vya maambukizi.

Hata hivyo serikali ya Kremlin imepuuza mara kadhaa wasiwasi huu ikisema kwamba Urusi imeweza kupunguza kasi ya mripuko huo na kuwahakikishia watu kwamba hatua zote zinazohitajika zimechukuliwa kuhakikishha usalama wa wapiga kura.

Putin ameongoza Urusi kwa miaka mingi

Putin ameshakaa madarakani kama rais na pia kama waziri mkuu katika kipindi cha miongo miwili iliyopita na ni kiongozi aliyetawala kwa kipindi kirefu zaidi nchini Urusi tangu Joseph Stalin aliyekuwa kiongozi wa Soviet.

Vituo vya kupigia kura katika uchaguzi huu wa mapema vilifunguliwa kote nchini humo ikiwa ni siku moja baada ya Urusi kuafanya gwaride kubwa lililohusisha wanajeshi 13,000 kusherehekea kumbukumbu ya miaka 75 ya kumalizika kwa vita vya pili vya dunia barani Ulaya.

Na katika tukio hilo Putin alitoa hotuba na kuutaja ushiriki wa vikosi washirika dhidi ya utawala wa wanazi nchini Ujerumani kama mbiu ya mema dhidi ya uovu. Hapana shaka mageuzi hayo ya katiba yanatarajiwa kuungwa mkono.