1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yafanya mashambulio mapya dhidi ya Ukraine

29 Mei 2023

Mashambulio ya Urusi yaendelea nchini Ukraine huku Waziri wa Mambo Nje wa Urusi, Sergei Lavrov akionya kuwa makubaliano ya usafirishaji nafaka hayataweza kuendelea bila ya kutimizwa makubaliano ya Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, ameyasema hayo akiwa ziarani jijini Nairobi nchini Kenya ambapo amesisitiza kuwa makubaliano hayo hayajatimizwa mpaka sasa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov.Picha: Vyacheslav Prokofyev/TASS/IMAGO

Makubaliano hayo juu ya mpango unaoruhusu usafirishaji salama wa chakula na mbolea katika Bahari Nyeusi yalifikiwa Julai mwaka jana ambapo Umoja wa Mataifa unatakiwa kuhakikisha Urusi haikabiliwi na vikwazo katika mpango huo wa usafirishaji wa nafaka na mbolea kwa kipindi cha miaka mitatu.

Wakati huo huo Ukraine imesema imedungua makombora yote ya Urusi yaliyorushwa nchini humo usiku wa kuamkia jumatatu katika wimbi la pili la mashambulizi ya Urusi.

Mkuu wa majeshi ya Ukraine, Valery Zaluzhny amesema jumla ya makombora 11 aina ya Iskander-M' na 'Iskander-K' yaliruhswa kutokea upande wa kaskazini mwa Ukraine.

Kwa upande wake wizara ya ulinzi ya Urusi imesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimezishambulia kambi za jeshi la Ukraine zilizolengwa na kuziharibu.

Urusi imeushambulia uwanja wa ndege wa kijeshi katika mkoam wa Magharibi wa Khmelnytskyi nchini Ukraine, ambapo ndege tano zimeharibiwa pamoja na barabara ya kurukia ndege, Gavana wa eneo hilo Serhyi Hamaliy ameongeza kusema kuwa mashambulizi hayo yalisababisha moto katika maghala ya karibu yanayohifadhi mafuta na vifaa vya kijeshi.

Mashambulizi ya makombora ya Urusi kutokea angani pia yalilenga maeneo tisa katika mkoa wa mashariki wa Donetsk, ikiwa ni pamoja na mji wa Kramatorsk ambao ni makao makuu ya jeshi la Ukraine, amesema Gavana wa eneo hilo Pavlo Kyrylenko.

Rais wa Ukraine Volodymiyr ZelenskyPicha: John Moore/Getty Images

Taarifa kutoka kwenye ofisi ya rais wa Ukraine zinafahamisha kwamba takriban raia watatu wamejeruhiwa nchini Ukraine kote katika mashambulizi hayo mapya.

Wakuu wa jeshi nchini Ukraime wamesema mfumo wa ulinzi wa anga katika jiji la Kiyv umefunguliwa baada ya jiji hilo kukabiliwa na mshambulio usiku wa kuamkia leo.

Kwingineko, makombora ya Urusi yalipiga kijiji kimoja huko kaskazini mashariki mwa mkoa wa Kharkiv. Watu sita wamejeruhiwa wakiwemo watoto wawili na mama mjamzito.

Mwanajeshi wa Ukraine katika mkoa wa Kharkiv.Picha: DIMITAR DILKOFF

Pia, mamlaka katika eneo la mashariki la Dnipropetrovsk, imesema mtu mmoja ameuawa kwenye mashambulizi mengine ya Urusi. Watu wengine tisa, wamejeruhiwa akiwemo mtoto wa miaka 11.

Msemaji wa jeshi la anga la Ukraine, Yurii Ihnat ameeleza kuwa makombora hayo yalirushwa kutokea upande wa kaskazini kwenye eneo la Urusi lililo umbali wa kilomita 380 kutoka kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine.

Vyanzo: AFP/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW