1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yafanya mashambulizi kutaka kuukamata mji wa Bakhmut

27 Desemba 2022

Vikosi vya Urusi vimeshambulia miji ya mashariki na kusini mwa Ukraine siku moja tu baada ya Sergei Lavrov kusema ni sharti Ukraine iyakubali matakwa ya Urusi ili kuvimaliza vita hivyo.

Kämpfer der Söldnergruppe Wagner in der Ukraine
Picha: Nicolas Cleuet/Le Pictorium/MAXPPP/dpa/picture alliance

Miongoni mwa matakwa hayo ya Urusi ni kwamba Ukraine ikubali waziwazi kuwa moja juu ya tano ya nchi yake ambayo Urusi inadai kuchukua sasa ni sehemu rasmi ya Urusi.

Lakini Ukraine ambayo inaungwa mkono na Marekani na vilevile washirika katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO, imeapa kupambana vikali kuyakomboa majimbo hayo na kuwafukuza wanajeshi wote wa Urusi kutoka kwenye ardhi yao.

Jeshi la Urusi limedai kusababisha maafa makubwa dhidi ya wanajeshi wa Ukraine katika uwanja wa mapambano Jumanne kuanzia Kherson iliyoko kusini mwa Ukraine hadi Kharkiv iliyoko kaskazini mashariki.

Lavrov: Magharibi na Ukraine zataka kuiangamiza Urusi

Shirika la habari la Urusi ambalo lilinukuu wizara ya Ulinzi ya Urusi limeripoti kwamba wanajeshi 60 wa Ukraine wameangamizwa kule Donetsk. Na kwamba katika jimbo Jirani las Luhansk, wanajeshi 30 wa Ukraine waliuawa.

Ukraine haijatoa kauli kuhusu madai hayo ambayo ni vigumu kuthibitisha.

Waziri wa Mambo ya Nje wa urusi Sergei Lavrov asema ni sharti Ukraine itekeleze matakwa yao ili kumaliza vita hivyo la sivyo jeshi la Urusi ndilo liamue suala hilo.Picha: Vitaliy Belousov/SNA/imago

Urusi yalenga mji wa kimkakati Bakhmut

Baada ya vikosi vya Urusi kushindwa kwa mfululizo katika baadhi ya maeneo tangu ilipoanzisha operesheni hiyo ya kijeshi nchini Ukraine, Urusi kwa sasa inalenga kukamata mji wa kiviwanda Bakhmut uliokuwa na wakaazi 70,000 kabla ya vita, lakini ambao sasa una wakaazi 10,000 pekee, wengi wakiwa wazee.

Udhibiti wa mji huo unaweza kuipa Urusi nafasi ya kusogea miji mingine mikubwa ya Kramatorsk na Sloviansk.

Jenerali mmoja wa jeshi la Ukraine amesema kwa muda wa saa 24 zilizopita, vikosi vya Ukraine vimeweza kuzuia mashambulizi kadhaa ya Urusi katika mkoa wa Luhansk na mengine sita eneo la Donetsk.

Ameripoti kwamba Urusi imefanya mashambulizi zaidi katika mji wa Kherson, Zaporizhzhia na katika majengo ya makaazi ya watu jimbo la Kharkiv, kaskazini mashariki mwa Ukraine karibu na mpaka wao na Urusi.

Ukraine yatuma tena ndege zisizo rubani ndani ya Urusi

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amesema katika hotuba yake ya hivi karibuni kuhusu hali ya vita nchini Ukraine, kwamba mapigano yamepamba moto karibu na mji wa kimkakati wa Bakhmut mkoa wa Donetsk na Syatove, kaskazini mwa Luhansk.

Donetsk na Luhansk ambazo huunda jimbo la kiviwanda la Donbas ni miongoni mwa majimbo ambayo Urusi inadai kwa sasa ni sehemu yake.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiri hali katika uwanja wa mapambano Donbas ni mbaya na ya kusikitisha.Picha: Ukrainian Presidency/abaca/picture alliance

Zelensky akiri hali ni ngumu katika uwanja wa mapigano Donbas

Wizara ya ulinzi ya Uingereza imeandika kwenye ukurasa wao wa Twitter kwamba Urusi imeendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara japo kwa kiwango cha chini katika maeneo hayo ya Bakhmut na Syatove.

Putin asema yuko tayari kwa majadiliano kuhusu Ukraine

Kanda ya video iliyonaswa na shirika la habari la Reuters ilionesha jengo kubwa la makaazi likiwaka moto mjini Bakhmut na majengo mengine yaliyoharibiwa.

Mnamo Jumatatu, Sergei Lavrov, waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi aliliambia shirika la habari la nchi hiyo TASS kwamba adui anafahamu matakwa yao ambayo ni kuachana na shughuli za kijeshi na kutokomeza "Unazi mamboleo” katika maeneo ambayo utawala wake unadhibiti, kuondoa vitisho dhidi ya usalama wa Urusi na kutambua sehemu mpya ilizochukua. Aliongeza kusema "la muhimu ni kuyatekeleza kwa manufaa yao, la sivyo mzozo huo utaamuliwa na jeshi la Urusi".

Katika hotuba yake ya kila siku, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alieleza kuwa hali katika uwanja wa mapambano jimbo la Donbas ni ngumu na ya kusikitisha.

Vyanzo: Rtre, Dpae

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW