1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yafanya mashambulizi makubwa katika miji ya Ukraine

20 Septemba 2023

Urusi imeendeleza mashambulizi nchini Ukraine ambako watu wawili wanaarifiwa kuuawa katika miji ya Lviv na Kherson. Kyiv imesema kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga imefanikiwa kudungua ndege 27 zisizo na rubani za Urusi.

Ukraine | Krieg | russischer Drohnenangriff auf Liwiw
Picha: Ukrainian Emergency Service/AP Photo/picture alliance

Maafisa wa Ukraine wamesema kuwa Urusi imefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani mapema leo asubuhi ambayo yamelenga maghala matatu katika mji wa magharibi wa Lviv na kusababisha moto mkubwa na kifo cha angalau mtu mmoja.

Gavana wa Lviv Maxim Kozitsky amesema kuwa vikosi vya zima moto vilijaribu kuudhibiti moto huo na kwamba kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26 amejeruhiwa. Kozitsky amesisitiza kuwa hakukuwa vifaa vyovyote vya kijeshi vilivyokuwa vikihifadhiwa katika maghala hayo, na kwamba katika jumla ya ndege zisizo na rubani 18 zilizorushwa na Urusi, 15 zilidunguliwa.

Jeshi la anga la Ukraine limesema katika mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo, Urusi ilituma nchini jumla ya ndege 30 zisizo na rubani na kombora moja la masafa marefu na kwamba ndege hizo 27 zilidunguliwa. Moscow haijazungumzia chochote juu ya taarifa hizo lakini imekuwa ikikanusha kuwalenga raia kimakusudi au miundombinu ya raia.

Moshi mweusi ukionekana katika mji wa Lviv ambao umeshambuliwa na vikosi vya Urusi: 19.09.2023Picha: Yuriy Dyachyshyn/AFP/Getty Images

Mamlaka za kijeshi katika mji wa kusini wa Kherson zimesema vikosi vya Urusi pia vimeushambulia mji huo na kumuua askari polisi mmoja na kuwajeruhi raia wawili.

Soma pia: Ukraine yasema imevunja ngome ya "adui" huko Bakhmut

Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akiwa nchini Ujerumani kuhudhuria mkutano wa Kundi la Ulinzi la Ukraine, amesema siku ya Jumanne kuwa mashambulizi ya kujihami ya Ukraine dhidi ya majeshi ya Urusi yanapiga hatua na kwamba wanajeshi wa Kyiv wamekuwa wakivunja ngome zilizoimarishwa za jeshi la uvamizi la Urusi.

Meli ya nafaka yaondoka katika Bandari ya Ukraine

Meli ya "Resilient Africa" ikiwasili katika Bandari ya Chornomorsk :16.09.2023Picha: REUTERS

Ukraine imesema leo Jumanne kuwa meli ya mizigo iliyosheheni nafaka imefanikiwa kuondoka katika bandari ya kusini mwa Bahari Nyeusi licha ya vitisho vya Urusi kutaja kuwa meli za kiraia zingeliweza kulengwa kijeshi. Moscow ilitoa onyo hilo baada ya kujiondoa mwezi Julai katika makubaliano ya usafirishaji nafaka za Ukraine yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki, na inekuwa ikizidisha mashambulizi kwenye miundombinu ya bandari za Ukraine.

Waziri wa miundombinu Oleksandr Kurakov ameandika kwenye mtandao wa kijamii kuwa Meli ya "Resilient Africa" yenye tani 3,000 za ngano imeondoka kwenye bandari ya Chornomorsk na inaelekea nchini Uturuki. Kurakov amebainisha kuwa meli hiyo pia ilikuwa imeingia katika bandari ya Ukraine wiki kadhaa zilizopita kupitia ukanda mpya ulioanzishwa, pamoja na meli nyingine ambayo itaondoka hivi karibuni kuelekea nchini Misri.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW