1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi yafanya mashambulizi Ukraine usiku kucha

Hawa Bihoga
26 Septemba 2024

Vikosi vya Ukraine vimedungua droni 66 na makombora 4 yaliyovurumishwa na Urusi katika mashambulizi ya usiku kucha. Miundombinu ya raia ikiwemo ile ya nishati imeshambuliwa pia na kusababisha maeneo kadhaa kusalia giza.

Ukraine, Kharkiw | Makaazi ya raia yalioharibiwa kwa mashambulizi.
Majengo ya makaazi ya raia Ukraine yalioharibiwa na mashambulizi ya Urusi.Picha: Ukrainian Presidential Press Office via AP/picture alliance

Jeshi la Ukraine limesema vikosi vya Urusi vimevurumisha droni 78 zilizotengenezwa Iran na makombora sita katika maeneo mbalimbali nchini humo kwenye mashambulizi yake ya usiku kucha. Katika mashambulizi hayo Ukraine ilifanikiwa kudungua droni 66 na makombora manne.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Ihor Klymenko kupitia mitandao ya kijamii ameongeza kwamba kufutia mashambulizi hayo mwanamke mmoja aliuwawa katika mji wa Odesa huku watu wengine wanane wakijeruhiwa katika shambulio la bomu la kutegwa.

Ndege kadhaa ziliharibiwa katika mji mkuu, Kyiv ambapo takriban magari 20 pamoja na miundombinu ya raia ikiwemo mabomba ya gesi yaliharibiwa vibaya.

Shirika la umeme Ukraine limesema maeneo kadhaa ya nchi yamesalia bila umeme kufuatia mashambulizi hayo ya usiku kucha kutoka kwa vikosi vya Urusi.

Soma pia:Urusi yavikomboa vijiji viwili magharibi mwa Kursk

Mmoja wa wakaazi wa Zaporizhzhia, Larysa Kryuchkova amesema walisikia sauti kubwa za milipuko karibu na makaazi yao.

''Mwanzo kulikuwa na mlipuko mmoja mkubwa, mbwa wetu anaogopa milipuko, hivyo nilimkimbilia."

Aliongeza kuwa lau kama asingeliwahi mapema asingeokoa mali yoyote baada ya mashambulizi kwenye nyumba yake.

"Mgongo wangu ulitapakaa damu na ulikuwa unauma. Lakini nilipata tena fahamu na kuanza kutambaa.'' Aliongeza Larysa.

Mapema leo asubuhi jeshi la anga Ukraine lilisema kwamba limerekodi kuvurumishwa kwa makombora kadhaa bila kutoa maelezo zaidi.

Kwa upande wake jeshi la Urusi katika taarifa yake mapema leo limesema limeuteka mji wa Ukrainsk ulio mashariki mwa Donetsk, ikiwa ni ushindi wake wa karibuni zaidi katika mkururo wa mafanikio yake kwenye uwanja wa vita.

Zelensky kuwasilisha "mpango wa ushindi" kwa Biden

Katika jitihada zake za kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa kutoka kwa washirika wake wa karibu Rais volodymyr Zelensky wa Ukraine, anatarajiwa kukutana na Rais wa Marekani Joe Biden na Makamu wake Kamala Harris ili kuwasilisha kile alichokiita "mpango wake wa ushindi".

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Ziara ya Zelensky katika Ikulu ya White House leo, inatazamiwa kuangazia kusaka uungwaji mkono zaidi wa Marekani, ingawa haijabainika ikiwa Washington itaridhia kwa Kyiv kutumia makombora ya masafa marefu yaliotengenezwa na Marekani hadi Urusi.

Soma pia:Biden: Mpango wa kuisaidia zaidi Ukraine utatangazwa Alhamisi

Mgombea wa urais kupitia chama cha Republican Donald Trum ambae anapambana na Kamala Harris wa Democratic alimshutumu kwa mara nyingine Rais Zelensky kwa kukataa kufanya makubaliano na Moscow akihoji juu Marekani kutoa mabilioni ya dola kwa Kyiv.

Katika mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa mataifa hapo jana Jumatano Rais Biden alimuarifu Rais Zelensky kwamba ameelekeza kuongezwa kwa msaada wa kiusalama kwa Ukraine ambao utatangazwa kwa umma baadae leo Alhamisi.