1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yafunga vituo vya utamaduni vya Ujerumani

Amina Abubakar /Angela Mdungu / afp
2 Septemba 2026

Urusi imetangaza kuwa itavifunga vituo vya utamaduni vya Ujerumani vya Goethe-Institut katika miji kadhaa nchini humo.

Russland Moskau 2026 | Schild des Goethe-Instituts an der Fassade
Urusi imefunga vituo vya utamaduni vya Ujerumani baada ya Berlin kutangaza kufunga ubalozi mdogo wa Urusi ulioko Bonn kufuatia shambulizi la Leipzig.Picha: Ramil Sitdikov/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov amesema hatua hiyo ni jibu baada ya Ujerumani kufunga kituo cha Russian House mjini Berlin na ubalozi mdogo wa Urusi mjini Bonn. Ujerumani ilifanya uamuzi huo kwa madai kuwa Urusi ilihusika na jaribio la shambulio la droni katika uwanja wa ndege wa Leipzig/Halle. 

"Ujerumani ina matawi ya Taasisi ya Goethe mjini Moscow, St. Petersburg na Yekaterinburg. Bila shaka yatafungwa baada ya kituo chetu cha utamaduni kufungwa Ujerumani. Ni hatua inayoeleweka, vinginevyo tunaweza kupoteza heshima yetu. Hatua tuliyochukua inaashiria mwisho wa uwepo wa utamaduni wa Ujerumani nchini Urusi, ambao uliendelea kuwepo licha ya matatizo yote yanayohusiana na Ukraine," alisema Lavrov.

Mapema Jumatano Ujerumani ilitangaza kuwa uchunguzi na taarifa nyingine za kijasusi zimethibitisha kuwa Urusi ilihusika na jaribio la shambulio la droni ambalo limeibua mzozo kati ya nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul ameelezea masikitiko yake kuhusu uamuzi huo, akisema taasisi ya Goethe-Institut imekuwa ikijenga daraja la mahusiano ya kitamaduni na kijamii kati ya wananchi wa Urusi na Ujerumani hata katika mazingira magumu.

Ujerumani yawatambua washukiwa wa shambulio la droni Leipzig

Wachunguzi wa Ujerumani wanadaiwa kuwabaini watu wawili wanaoshukiwa kuhusika na jaribio la shambulio la droni katika Uwanja wa ndege wa Leipzig/Halle mwezi Agosti mwaka 2026

Mmoja ya maafisa wa usalama akiwa katika uwanja wa ndege wa Ujerumani wa Leipzig/ Halle baada ya shambulio la droni linalodaiwa kufanywa na UrusiPicha: Axel Schmidt/REUTERS

Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa leo Jumatano (02.09.2026)  na gazeti la Süddeutsche Zeitung pamoja na vituo vya utangazaji vya umma vya NDR na WDR, mmoja wa washukiwa ametambuliwa kuwa na asili ya kirusi mwenye pasipoti ya Latvia. Mshukiwa wa pili ni raia wa Belarus anayemiliki pasipoti ya Urusi.

Hapo Jana Jumanne, (01.09.2026) serikali ya Ujerumani ilisema inaamini kuwa Urusi ilihusikana jaribio hilo lililolenga ndege ya mizigo ya Ukraine katika uwanja huo wa ndege mapema mwezi uliopita.

Berlin yatishia hatua kali baada ya shambulio la Leipzig 

Ujerumani imeonya kuwa kutakuwa na majibu makali kufuatia kile ilichokiita shambulio la mseto na pia imetangaza kufungwa kwa ubalozi mdogo wa Urusi ulioko Bonn pamoja na taasisi ya kitamaduni ya Urusi ya "Russian House" mjini Berlin.  Berlin inaamini taasisi hiyo imehusika katika shughuli za ujasusi.

Hata hivyo, Urusi imekanusha kuhusika kwa namna yoyote katika tukio hilo la Leipzig. Tayari Moscow imemuita balozi wa Ujerumani nchini Urusi kutoa maelezo kuhusu kile ilichokitaja kuwa hatua za Berlin zenye msimamo wa kupinga Urusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW