Urusi yafungua tena ubalozi wake nchini Burkina Faso
29 Desemba 2023Wizara ya mambo ya nje ya Burkina Faso imethibitisha kwamba Urusi ilifungua rasmi ubalozi wake mjini Ouagadougou siku ya Alhamisi.
Soma pia:Burkina Faso ni adui wa sera za Ufaransa, si watu wake
Balozi wa Urusi nchini Ivory Coast, Alexei Saltykov, amesema ataongoza ubalozi huo wa Burkina Faso hadi balozi mpya atakapotajwa na kuitaja nchi hiyo kama "mshirika wa zamani mwenye uhusiano thabiti na wa kirafiki".
Saltykov asema uhusiano kati ya Urusi na Burkina Faso haujawahi kukatika
Saltykov ameongeza kuwa licha ya kutokuwepo kwa ubalozi wa Urusi nchini humo, ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za kisiasa na kiuchumi haujawahi kukoma.
Kufunguliwa kwa ubalozi wa Urusi nchini Burkina Faso kutaimarisha ushirikiano
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema kuwa kufunguliwa kwa ubalozi huo "kutaongeza uratibu katika masuala ya sera za kigeni" na kuimarisha "urafiki" kati ya nchi hizo mbili.
Urusi imezidi kutengwa kimataifa tangu kuanzisha vita vyake nchini Ukraine na katika miezi ya hivi karibuni imejadili ushirikiano mkubwa wa kijeshi na Burkina Faso.