Urusi yaifyatulia Ukraine makombora 30
18 Mei 2023Mashambulizi ya Urusi yanafanyika wakati jeshi la Ukraine likisema limepiga hatua kubwa katika mapambano makali yanayoendelea kushuhudiwa katika mji wa Bakhmut. China imeendelea kushinikiza hatua za kidiplomasia katika kuumaliza mzozo huo.
Mashambulizi ya Urusi katika jengo la kiwanda katika eneo la Odesa kusini mwa Ukraine, yamesababisha kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wawili, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa utawala wa kijeshi kwenye eneo hilo, Serhiy Bratchuk.
Soma Zaidi: Urusi yafanya mashambulizi makubwa ya makombora katika mji wa Kiev
Milipuko mikubwa ilisikika pia katika mji mkuu Kyiv, wakati vikosi vya Urusi vikiendelea kuulenga mji huo kwa mara ya tisa mwezi huu, na kuchukuliwa kama ishara ya wazi ya kuongezeka kwa mzozo baada ya wiki kadhaa za kushuhudiwa utulivu na wakati ambapo Ukraine ikitarajiwa kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza kwa kutumia silaha mpya na za kisasa ilizopewa na mataifa ya magharibi.
Mmoja ya wakazi katika mji wa Kyiv, Nataliia Yuriivna amesema walisikia milipuko na walipoamka asubuhi walikuta baadhi ya maeneo yameharibiwa vibaya na makombora hayo na wanachokifanya sasa ni kusafisha na kuondoa kila uchafu unaoweza kuleta madhara.
"Majira ya saa 12 asubuhi lililipuka, sijui ni droni ama kitu kingine... likachimba shimo hili. Nilitoka na mbwa wangu asubuhi nikakuta magari mengi ya kubebea wagonjwa na watoa huduma zote walikuwa hapa. Kwahivyo tukapasafisha. Na mchanga utaondolewa kwa sababu kuna vipande vya mizinga.. na hapa kuna watoto.." alisema mkaazi huyo.
Mkuu wa vikosi vya Ukraine Jenerali Valerii Zaluzhnyi amesema kupitia Telegram kwamba vikosi vyake vilifanikiwa kuyadungua makombora yaliyorushwa na Urusi kutokea baharini, angani na ardhini, yaliyolenga maeneo kadhaa ya Ukraine na yaliyorushwa kati ya saa tatu usiku wa jana hadi saa kumi na moja za alfajiri.
Tukisalia Kyiv, jeshi la Ukraine limesema limefanikiwa pakubwa kusonga mbele katika mapigano makali yanayoshuhudiwa katika mji wa Bakhmut, mashariki wa nchi hiyo, licha ya upungufu wa silaha na wanajeshi ikilinganishwa na vikosi vya Urusi. Msemaji wa jeshi Serhiy
Cherevatyi amesema kupitia televisheni kwamba licha ya upungufu huo, lakini wanajeshi wake wamepiga hatua kubwa, ingawa hakufafanua zaidi.
Wiki chache zilizopita, Kyiv ilisema imewaongezea shinikizo wanajeshi wa Moscow walioko eneo la kaskazini na kusini mwa Bakhmut, huku wapiganaji wa kundi la Wagner la Urusi nao wakisema wanazidi kuchanja mbuga na kuingia mjini humo.
Soma Zaidi:Ukraine yapongeza mafanikio ya kwanza kuelekea mji wa mapambano wa Bakhmut
China na Afrika kushinikiza zaidi suluhu ya amani.
Na huko Beijing taarifa zinasema mjumbe maalumu wa mahusiano ya Ulaya na Asia wa nchini China amesema akiwa ziarani huko Ukraine kwamba taifa hilo linataka kurejesha amani kati ya Urusi na Ukraine. Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya China imesema mjumbe huyo Li Hui alizungumzia suala la suluhu ya kisiasa, kuelekea mzozo huo, alipozungumza na rais Volodymyr Zelensky na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini.
Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje ya Ukraine Dymitro Kuleba amesisitiza jana kwamba hawatakubaliana na pendekezo lolote litakalopelekea kupoteza maeneo yao ama kuuweka mzozo huo katika hali ya mkwamo.
Huku hayo yakiendelea, ikulu ya Kremlin imesema leo kwamba ujumbe wa mataifa ya Afrika unaotaraji kuwasilisha mkakati wao wa kuumaliza mzozo huo utawasili kesho mjini Moscow. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Psekov amesema Moscow itakuwa tayari kusikiliza pendekezo lolote litakalosaidia hilo kufikiwa.