Urusi yaikabidhi Ukraine miili ya wanajeshi waliouawa vitani
9 Aprili 2026
Mara kwa mara pande hizo mbili hasimu zimekuwa zikibadilishana miili ya wanajeshi waliouwawa vitani, ikiwa ni sehemu ya makubaliano madogo katika mgogoro huo unaoendelea na uliosababisha mauaji ya maelfu ya watu tangu ulipoanza Februari 24 mwaka 2022.
Video ya shirika la Ruptly linalomilikiwa na serikali ilionyesha wanaume waliokuwa wamevalia nguo za buluu na glavu nyeupe, wakibeba mifuko mikubwa meupe ya kuhifadhia maiti ikihamishwa kutoka kwenye gari moja hadi jengine. Miili hiyo inadaiwa kuhamishwa chini ya uangalizi wa Shirika la Msalaba Mwekundu.
Makao makuu ya uratibu wa hali ya wafungwa wa kivita ilithibitisha kupitia mtandao wake wa kijamii kwamba miili 1000 waliopokea ilikuwa ni wa wanajeshi wa Ukraine. Kyiv imewahi kuituhumu Moscow kukabidhi miili ya wanajeshi wa Urusi waliouawa vitani ikidai ni wanajeshi wa Ukraine. Ukraine imesema baada ya miili hiyo kutambuliwa itapelekwa kwa familia zao kwa maziko.
Vita hivyo vya Urusi na Ukraine, viliuanzisha mgogoro mbaya kuwahi kushuhudiwa barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia, huku mamilioni ya watu wakipoteza makaazi yao, pamoja na mauaji ya maelfu ya raia yakiripotiwa katika pande zote mbili.
Manowari za Urusi zazuiwa kufanya operesheni ya 'uhalifu'
Kwengineko Uingereza na Norway na mataifa mengine yalishiriki operesheni ya wiki nzima, kuzuwia manowari za kijasusi za Urusi kufikia nyaya za chini ya maji katika eneo la kaskazini mwa eneo la Atlantiki, zikiishutumu Urusi kutumia vita vya Iran kupanga shughuli za uchochezi dhidi ya Ulaya.
Kulingana na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza John Healey, operesheni hiyo ilihusisha meli ya kivita ya Jeshi la Wanamaji la Uingereza, ndege na mamia ya wanajeshi, na ilifanikiwa kuzuia manowari za Urusi kufanya shughuli alizozitaja kuwa za kihalifu.
Aliongeza kuwa vyombo hivyo vya Urusi hatimaye viliondoka baada ya operesheni iliyodumu zaidi ya mwezi mmoja. Mataifa ya NATO yamekuwa yakionya mara kwa mara kuhusu hatari ya Urusi kuhujumu nyaya za mawasiliano ya kimataifa chini ya bahari, madai ambayo Moscow imekuwa ikiyakanusha.
Kundi la Memorial laidhinishwa kama kundi la kigaidi
Huku hayo yakiarifiwa Mahakama ya juu ya Urusi imeliweka katika orodha ya wahalifu kundi la kutetea haki za binaadamu la Memorial lililowahi kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel, Hatua hiyo ni sehemu ya kamata kamata inayoendelea dhidi ya wapinzani na mashirika ya kiraia nchini humo huku huku vita vya taifa hilo na Ukraine vikiendelea kushika kasi.
Kufuatia shauri la faragha lililosikilizwa hii leo mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo kulingana na ombi la wizara ya sheria iliyotaka shirika hilo kuidhinishwa kama kundi la kigaidi huku shughuli zake zikipigwa marufuku nchini Urusi.
Awali kundi hilo la Memorial lilipinga madai hayo lakini uamuzi uliotolewa unaipa nguvu mamlaka kudhibiti miradi yoyote ya kundi hilo pamoja na wafuasi wake. Shirika hilo ni moja ya shirika kongwe na mashuhuri linalotetea haki za binaadamu Urusi na lilikabidhiwa tuzo ya amani ya nobel ya mwaka 2022 ikiwa ni chini ya mwaka mmoja tangu uvamizi wa Urusi ulipoanzishwa dhidi ya Ukraine.
Kamati ya Nobel imeukosoa uamuzi huo ikisema ni ukiukaji wa maadili ya utu na uhuru wa kujieleza huku ikiitolea mwito Urusi kuacha mara moja unyanyasaji wa kundi hilo na wanachama wake.