Urusi yaionya Korea Kusini kuhusu mzozo wa Ukraine
19 Aprili 2023Korea Kusini ambayo ni mshirika wa Marekani imeipatia Ukraine misaada ya kibinadamu lakini hadi sasa ilikuwa imeondoa uwezekano wa kupeleka misaada ya kijeshi. Lakini rais wa taifa Yoon Suk Yeol amenukuliwa leo akisema kuwa "kama kutakuwa na hali ambayo haiwezi kupuuzwa na jumuiya ya kimataifa, kama vile shambulio kubwa dhidi ya raia" basi itakuwa vigumu kwa taifa hilo kusisitiza tu juu ya misaada ya kiutu au kifedha. Msemaji wa rais wa Urusi Dmitry Peskov amesema kuwa.
"Kwa masikitiko yetu, Seoul imechukua msimamo usio wa kirafiki katika hadithi yote hii. Huu ni mwendelezo. Hakika nchi za magharibi zitajaribu kuvuta nchi zaidi na zaidi moja kwa moja katika mzozo huu. Kuanza kupeleka silaha kutamaanisha kujihusisha kusiko moja kwa moja katika mzozo huu."
Soma pia: Urusi yaushambulia mkoa wa Odesa kwa ndege za Drone
Mapema leo pia Rais wa Ukraine amekagua mipaka ya Belarus na Poland na kuwashukuru walinzi wa mipaka hiyo kwa ajili ya ulinzi tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi. Kiongozi huyo amechapisha mkanda wa video kupitia mtandao wa Telegram ukimwonyesha alipokutana na walinzi katika pori na uzio wa waya kando ya mto ulioko kwenye mkoa wa Volyn Kaskazini Mashariki mwa Ukraine.
Soma: Urusi yaushambulia mkoa wa Odesa kwa ndege za Drone
Wakati huo huo, vikosi vinavyoungwa mkono na Urusi katika mkoa wa mashariki mwa Ukraine wa Donetsk vimedai kwamba vikosi vya Ukraine vimelipua majengo manne ya makaazi ya raia katika mji wa Bakhmut siku mbili zilizopita na kuwaua watu 20, kulingana na taarifa ya shirika la habari la TASS. Katika hatua nyingine, shirika la usalama wa ndani la Urusi FSB, limemkamata mtu mwenye uraia wa Urusi na Ukraine anayeshukiwa kupanga "hujuma" dhidi ya kituo cha miundombinu ya nishati katika eneo lililonyakuliwa la Crimea. Wabunge wa Urusi wiki hii walizidisha adhabu kali kwa "ugaidi" na hujuma huku Moscow ikiendeleza mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya Ukraine.
Na serikali ya Bulgaria imeidhinisha marufuku ya muda katika uagizaji wa nafaka za Ukraine pamoja na bidhaa nyingine za vyakula baada ya Hungary nayo kupanua wigo wa marufuku yake na kujumuisha vyakula zaidi. Katika siku za hivi karibuni, Poland, Hungary na Slovakia zilitangaza kuzuia uagizaji wa nafaka na vyakula vingine kutoka Ukraine iliyokumbwa na vita baada ya anguko la bei kulikosababishwa na maandamano ya wakulima. Mnamo mwezi Mei mwaka uliopita, Umoja wa Ulaya uliruhusu Kyiv kusafirisha hifadhi yake ya nafaka kupitia muungano huo baada ya kufungwa kwa njia ya usafirishaji ya Bahari Nyeusi.