1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Watu saba wauawa na zaidi ya 50 kujeruhiwa nchini Ukraine

31 Julai 2023

Urusi imeshambulia tena miji ya Kusini mwa Ukraine leo asubuhi na kuwauwa takriban raia saba na kuwajeruhi zaidi ya 50 wengine. Haya ni kwa mujibu wa mamlaka katika mkoa wa Kherson

Ukraine Kryvyi Rih | Einschlag einer Rakete
Picha: Ministry Press Office/AP Photo/picture alliance

Katika mji wa Kryvyi Rih, makazi ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, makombora mawili ya Urusi yalilenga jengo la ghorofa 9 na lingine la chuo kikuu mapema leo. Mkuu wa jeshi katika eneo hilo Oleksandr Vilkul, amesema takriban watu watano akiwemo mama mmoja na bintiye wa umri wa miaka 10 walifariki dunia na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Mamlaka ya eneo hilo inaamini kuwa watu zaidi huenda wamekwama chini ya majengo yote mawili. Kanda ya video inaonesha jengo hilo la ghorofa lililolengwa likiteketea kwa sehemu na likiwa katika hatari ya kuanguka. Hata hivyo shughuli ya uokoaji inaendelea.

Ukubwa wa mashambulizi dhidi ya Ukraine yaongezeka kwa kiasi kikubwa

Akizungumzia shambulizi hilo, waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema wakati ambapo kuna juhudi zilizotibuka za mashambulizi yanayoitwa ya kulipa kisasi, serikali ya Kyiv, kwa msaada wa wafadhili wa Magharibi, ililenga kufanya mashambulizi ya kigaidi kwenye miundombinu ya kiraia katika miji ya Urusi na kuongeza kuwa kwa kuzingatia hali ya sasa, hatua za ziada zimechukuliwa ili kuongeza ulinzi dhidi ya mashambulizi ya angani na baharini. Ukubwa wa mashambulizi hayo dhidi ya vituo vya kijeshi vya Ukraine, ikijumuisha wale wanaounga mkono mashambulizi hayo ya kigaidi umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei ShoiguPicha: KCNA/REUTERS

Kupitia mtandao wa kijamii wa telegram, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa risala zake za rambirambi kwa wahanga wa mashmabulizi hayo na kulaani kitendo hicho cha Urusi. Zelensky amesema maeneo ya Ukraine yanalengwa na wavamizi wanaoendelea kutishia miji na watu wenye amani.

Dhamana ya ulinzi ya mataifa mawili kwa Ukraine, itatatiza vigezo vya mahusiano ya kimataifa

Katika hatua nyingine, msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amedai kuwa uwezekano wa  dhamana ya ulinzi ya mataifa mawili kwa Ukraine, itatatiza vigezo vya mahusiano ya kimataifa na haipaswi kufanyika kwa kupuuza mahitaji ya Urusi. Peskov amesema leo kuwa kwa maoni yao, hili litachangia kudorora zaidi kwa hali ya usalama barani Ulaya.

Mara kwa mara, Urusi imerejelea kuwa usalama wake unahatarishwa na malengo ya Ukraine ya kujiweka karibu na mataifa ya Magharibi ikiwa ni pamoja na kujiunga na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya kujihami ya NATO, ambayo imesisitiza mara zote kwamba haileti tishio lolote la usalama kwa Urusi. Ukraine inatarajia kuanza mazungumzo wiki hii na Marekani kuhusu dhamana za ulinzi kabla ya kujiunga na jumuiya ya NATO baadaye.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW