Urusi yaishambulia miundo mbinu ya nishati ya Ukraine
27 Agosti 2025
Urusi na Ukraine zimeendelea kushambuliana kwa droni, wizara ya nishati ya Ukraine imesema kwamba, mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo ya Urusi yamelenga mioundo mbinu ya nishati ya nchi hiyo katika mikoa sita.
Mashambulio ya Urusi yamelenga miundo mbinu ya kusafirisha nishati ya mafuta na gesi katika mikoa ya sita ambayo ni pamoja na Poltava na Sumy ambako uharibifu mkubwa umefanyika.
Vituo vikubwa vya uzalishaji gesi nchini Ukraine viko hasa kwenye mikoa ya Poltava na Kharkiv na gavana wa Poltava Volodymyr Kohut amesema shambulio la Droni la Urusi lilisababisha kukatika kwa umeme kwa muda katika eneo hilo na baadae hali ilirekebishwa.
Umeme ulikatika pia katika baadhi ya sehemu za mji wa Kaskazini wa Sumy. Lakini Ukraine nayo imeishambulia Urusi kwa Droni huku vifusi vya droni iliyodunguliwa na kushika moto vikiangukia kwenye paa la jumba moja katika mji wa Kusini mwa Urusi wa Rostov-On Don, na kulazimisha kuhamishwa kwa wakaazi 15.Soma pia: Urusi yazilaumu nchi za Ulaya kutaka "kuzuia" mchakato wa amani
Kufuatia mashambulio yanayoendelea hivi sasa baina ya nchi hizo mbili rais wa Marekani Donald Trump ametowa onyo kwa Urusi hapo jana akisema yuko tayari kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi hiyo ikiwa rais Vladmir Putin atashindwa kukubali kusitisha vita.
"Ningetaka vita visitishwe.Na vita hii haiwezi kuwa ya dunia lakini itakuwa ni ya kiuchumi. Na vita ya kiuchumi itakuwa mbaya na itakuwa mbaya zaidi hasa kwa Urusi.Na sitaki iwe hivyo.Sasa itabidi nitazame,kwasababu unajuwa pia hata Zelensky ana mapungufu''
Rais Zelensky hivi leo amesema umewadia wakati wa kuandaliwa mazungumzo ya viongozi juu ya masuala ya kupewa kipaumbele na ratiba ya mwisho ya muda wa kufikiwa mpango utakaoihakikishia usalama nchi yake.
Ukraine ambayo imeongeza mashambulio yake yanayolenga ndani ya Urusi katika miezi ya hivi karibuni, imesema hatua yake imekuwa ni ya kuijibu mashambulio ya Urusi ambayo imeendelea kwa kipindi chote kuishambulia Ukraine.
Pande zote mbili, Kiev na Moscow zimekanusha kuwalenga raia kwenye vita hivi vilivyoanzishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Februari mwaka 2022. Viongozi wa Ulaya akiwemo Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wamekuwa wakiishinikiza Urusi kuacha hila za kujaribu kuchelewesha juhudi za kukutana na Zelensky kumaliza vita hivi.Soma pia: Urusi yasema Ukraine imekishambulia kinu cha nyuklia
Kansela huyo pamoja na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na waziri mkuu wa Poland Donald Tusk wanapanga hivi leo kuitembelea Moldova ambayo inapakana kabisa na Ukraine.
Kama ilivyo Ukraine Moldova imekuwa ikitaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2022, lakini imegawika kati ya wanaogemea Brussels na wanaoiunga mkono Urusi.
Viongozi hao wanataka kuonesha uungaji mkono wao kwa Rais Maia Sandu na serikali yake inayoegemea upande wa Brussels kabla ya uchaguzi wa bunge mwezi Septemba.