1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yaituhumu Ukraine kwa mashambulizi mjini Moscow

1 Agosti 2023

Urusi imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani katika mji mkuu Moscow ambapo majengo kadhaa yamelengwa. Kremlin imesema hatua kadhaa zimechukuliwa kuboresha ulinzi.

Russland Moskau | Zerstörung nach Drohnenangriff
Picha: AP Photo/picture alliance

Jengo la ghorofa kunakopatikana ofisi za wizara tatu mjini Moscow limeshambuliwa tena hii leo ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha siku mbili zilizopita. Urusi imeishutumu Ukraine kwa mashambulizi hayo katika ardhi yake.

Maafisa wa Urusi wamedai hatua ya Ukraine kuzidisha mashambulizi mjini Moscow inaonesha kushindwa kwake katika mpango wake wa kuchukua udhibiti wa maeneo yaliyonyakuliwa na Moscow huku kauli ya wiki iliyopita ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ikibaini kuwa "taratibu vita vinarejea ndani ya Urusi".

Vikosi vya zima moto mjini Moscow vikiwasili katika Jengo la ghorofa lililoshambuliwa kwa ndege zisizo na rubani (30.07.2023)Picha: Mikhail Tereshchenko/ITAR-TASS/IMAGO

Siku ya Jumanne, mshauri wa Zelensky Mykhailo Podolyak, ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twiter kwamba Moscow imeanza sasa kuzoea matokeo ya vita kamili bila hata hivyo kuthibitisha au kukana kuhusika kwa Kyiv katika mashambulizi hayo.

Serikali ya Urusi imesema Wizara yake ya ulinzi itatekeleza jukumu lake na kuchukua hatua zaidi za ulinzi kufuatia shambulio hilo mpya la ndege isiyo na rubani katika mji wa Moscow. Msemaji wa Ikulu wa Kremlin Dmitry Peskov amekiri kuwepo hatari ya mashambulizi:

" Sina la kuongeza kwa yale ambayo Wizara ya Ulinzi tayari imesema. Jana niliweka wazi kwamba ni wanajeshi pekee wanaoweza na wanaopaswa kutoa maoni juu ya hili maana wana maoni ya kitaalam. Kwa hakika, tishio lipo, ni dhahiri, na hatua zinachukuliwa."

Msemaji wa Ikulu wa Kremlin Dmitry PeskovPicha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Mashambulizi huko Moscow na katika rasi ya Crimea, iliyonyakuliwa kinyume cha sheria na Urusi mwaka 2014, yanafuatia shambulio baya la Urusi dhidi ya Kryvyi Rih, mji ulio katikati mwa Ukraine na alikozaliwa rais Zelensky.

Mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani katika ardhi ya Urusi, yanadhihirisha  udhaifu wa Moscow  wakati uvamizi wake nchini Ukraine ukiingia mwezi wa 18.

Urusi yashambuliwa pia katika Bahari Nyeusi

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema hii leo kuwa imezuia mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani za Ukraine yaliyokuwa yakilenga meli zake za kiraia na zile za jeshi la wanamaji katika Bahari Nyeusi.

Soma pia: Ukraine yazishambuliwa Moscow, Crimea kwa droni

Aina tofauti ya ndege zisizo na rubani (droni).Picha: JULIEN DE ROSA/AFP

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema imezidungua ndege mbili zisizo na rubani nje ya Moscow na kusisitiza kuwa vikosi vya Ukraine vilijaribu shambulio lililozimwa dhidi ya Meli za Vasiliy Bykov na Sergei Kotov na boti zingine tatu katika Bahari Nyeusi.

Wizara hiyo imebaini kuwa meli hizo mbili zilikuwa katika harakati ya kudhibiti usafirishaji baharini kusini-magharibi mwa Sevastopol na kwamba zingeendelea na jukumu hilo.

Soma pia: Papa Francis aiomba Urusi kurudi kwenye makubaliano ya nafaka

Hayo yakiarifiwa, Iceland imesema siku ya Jumanne kuwa imesitisha shughuli katika ubalozi wake nchini Urusi, ikiwa ni nchi ya kwanza ya Ulaya kuchukua hatua hiyo kwani uhusiano wa kibiashara, kitamaduni na kisiasa umedorora.Nchi hiyo ya Nordic ilitangaza mwezi Juni mwaka huu kuwa itaufunga Ubalozi wake huko Urusi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW