1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yajiandaa kukabiliana na mashambulizi ya Ukraine

28 Aprili 2023

Wakati Urusi wakijaribu kujizatiti na kuimarisha mifumo yao ya ulinzi nchini Ukraine, Kyiv kwa upande wao wanajiandaa kwa mashambulizi makubwa katika mji wa Polohy na maeneo mengine kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Ukraine Bachmut | Satellitenbilder der Firma Maxar | Zerstörungen in und bei Bachmut | JANUAR 2023
Picha: Maxar Technology/Handout via REUTERS

Ngome za ulinzi zilizoonekana katika picha za satelaiti zilizonaswa na shirika la Capella Space ni sehemu ya mtandao mkubwa wa ngome za Moscow kutoka eneo la magharibi mwa Urusi hadi mashariki mwa Ukraine. Ngome hizo zinaendelea hadi Crimea ili kujiandaa na shambulio kubwa la vikosi vya Ukraine.

Maelfu ya wanajeshi wa Ukraine wamepewa mafunzo katika nchi za Magharibi, ya jinsi ya kutumia vifaa tofauti vya kijeshi kwenye uwanja wa vita, na kulingana na maafisa wa Ukraine, mashambulizi hayo yatafanyika wakati majeshi yake yatakapokuwa tayari.

Shirika la habari la Reuters limekagua picha za satelaiti zinazoonyesha maelfu ya ngome za ulinzi ndani ya Urusi na katika mstari wa mbele vitani nchini Ukraine na kubaini kuwa mkoa wa kusini wa Zaporizhia na lango la rasi ya Crimea ndivyo vinavyolindwa mno na Urusi.

Mtazamo wa wataalamu

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: president.gov.ua

Wataalamu sita wa masuala ya kijeshi wamesema ngome hizo za ulinzi za Urusi kwa kiasi kikubwa zilijengwa kutokana na mafanikio ya haraka ya Ukraine, na kwamba hilo kwa wakati huu linaweza kuipa kibarua kigumu zaidi Ukraine. Kwa sasa mafanikio ya Ukraine yatategemea uwezo wake wa kuendesha kwa ufanisi operesheni mahsusi.

Soma pia: Zelensky asema Urusi inawaua raia bila huruma kwenye jimbo la Kherson

Neil Melvin, mchambuzi katika Taasisi ya Royal United Services anasema muhimu ni kwa Ukraine kufahamu iwapo itaweza kufanya aina hii ya vita kwa kujumuisha operesheni ya pamoja ya silaha. Melvin ameendelea kusema kuwa Warusi wameonyesha kuwa hawawezi kuendesha vita vya aina hiyo na ndiyo maana wamerejea katika mifumo yao ya zamani ya vita iliyotumiwa enzi ya Soviet ambayo hulenga kwanza kumdhoofisha adui.

Wanajeshi wa Ukraine wakifyatua kombora huko KhersonPicha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Mashambulizi ya Ukraine yanaweza kubadili muelekeo wa vita ambao kwa sasa vimekuwa ni vita vya umwagaji damu na vya kumdhoofisha adui ambapo wataalam wa masuala ya kijeshi wanasema hilo huenda likadhohofisha safu ya ulinzi ya Urusi.

Ikiwa Kyiv itaweza kurejesha udhibiti wa eneo lake la kusini, inaweza tena kuzitumia kikamilifu njia zake za usafirishaji kuelekea Bahari Nyeusi wakati ambapo Urusi imetangaza kuwa huenda ikafunga njia za usafirishaji nafaka.

Wataalam wa kijeshi wanasema kwa hivi karibuni, huenda Ukraine isipokee msaada mwingine mkubwa wa vifaa vya kivita kutoka Mataifa ya Magharibi na hilo linaweza kuwa shinikizo kubwa kwa Kyiv kuweza kuchukua tena udhibiti wa maeneo yake. Wizara ya Ulinzi ya Ukraine haikueleza chochote kuhusu mashambulizi hayo.

Ukanda wa ardhini

Rais wa Urusi Vladmir Putin akifanya ziara huko Kherson (18.04.2023)Picha: Russian President Press Office/dpa/picture alliance

Ukraine imeapa kurejesha eneo lote lililonyakuliwa na Urusi, ambalo linakaribia ukubwa wa nchi ya Bulgaria, lakini maafisa wa Ukraine wamekuwa wakisita kufichua habari yoyote ambayo inaweza kusaidia Moscow.

Mataifa ya Magharibi yametuma vifaa vya kisasa vya kivita na vifaru vinavyoweza kutumiwa katika mashambulizi kama hayo. Na ndiyo sababu Urusi imekuwa ikiandaa ngome zake za ulinzi ili kuhakikisha wanajeshi wake wanakuwa salama tofauti na walipofurushwa kutoka eneo la kaskazini-mashariki mwa Ukraine nakatika mji wa Kherson.

Soma pia: Ukraine: Putin azuru mikoa miwili inayokaliwa na Urusi

Picha za satelaiti zilizokaguliwa na shirika la habari la Reuters zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya ujenzi wa ngome hizo ulifanyika baada ya mwezi Novemba mwaka 2022, wakati vikosi vya Moscow vilipolazimika kuondoka katika mji wa wa kusini wa Kherson huku vikilenga pia kuimarisha ulinzi wao katika msimu wa baridi.

Wiki iliyopita, Rais wa Urusi Vladimir Putin alifanya ziara adimu huko Kherson katika kile ambacho baadhi ya waangalizi wamesema ni ishara ya kudhihirisha umuhimu wa kimkakati wa eneo hilo. Naye Oleksandr Musiyenko, mchambuzi wa kijeshi huko Kyiv, amesema eneo la kusini mwa Ukraine ni muhimu kimkakati kwa nchi hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW