1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakabiliwa na shinikizo

15 Machi 2018

Urusi imeonya hii leo kwamba italipiza kisasi hivi karibuni hatua ya Uingereza kuwafukuza wanadiplomasia wake 23, kufuatia shambulizi la sumu inayoshambulia mishipa ya fahamu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi.

Sergei Lawrow russischer Außenminister
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Urusi imeonya hii leo kwamba italipiza kisasi hivi karibuni hatua ya Uingereza kuwafukuza wanadiplomasia wake 23, kufuatia shambulizi la sumu inayoshambulia mishipa ya fahamu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi. Uingereza ilidai kwamba Urusi inahusika na shambulizi hilo la sumu dhidi ya jasusi huyo Sergei Skripal na binti yake Yulia katika mji wa Salisbury nchini Uingereza.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa hii leo, Uingereza, Marekani, Ufaransa na Ujerumani wamelaani shambulizi hilo la sumu dhidi ya jasusi huyo wa zamani wa Urusi na kuituhumu Urusi kwa kufanya shambulizi hilo, na kuitaka Urusi kutoa taarifa kamili ya mpango wa sumu aina ya Novichok kwa shirika la kudhibiti silaha za sumu.

Jasusi huyo pamoja na binti yake bado wanaelezwa kuwa katika hali mbaya hospitalini, tangu walipobainika Machi 4. 

Urusi imekana kuhusika kwa namna yoyote na waziri wake wa mambo ya nje, Sergei Lavrov aliituhumu Uingereza kwa kutumia ubabe, na kuongeza kuwa hii kwa sehemu imetokana na matatizo yanayoyakabili Uingereza kutokana na mipango yake ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ifikapo mwakani.

Lavrov amesema, Urusi itajibu mapigo hivi karibuni lakini maafisa wa Uingereza watajulishwa kwanza, ripoti inayokinzana na iliyotolewa awali na shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA, iliyosema Lavrov aliahidi kuwafukuza wanadiplomasia wa Uingereza waliopo nchini humo. Lakini pia, amesema, huenda shambulizi hilo lilikuwa na nia ya kuvuruga maandalizi ya Urusi ya kombe la soka la dunia.  

Askari wakiwa wamevaa vifaa vya kujilinda na gesi ya sumu wanapoendelea kuchunguza shambulizi hiloPicha: Getty Images/C.J. Ratcliffe

Ikiwa ni idadi kubwa ya wanadiplomasia waliofukuzwa Uingereza tangu kumalizika kwa vita baridi, waziri mkuu wa Uingereza Theresa May hapo jana Jumatano aliwapa wiki moja ya kuondoka raia 23 wa Urusi ambao alisema walikuwa majasusi waliofanya majukumu yao chini ya mwamvuli wa wanadiplomasia.

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov kwenye mkutano kwa njia ya simu amenukuliwa akisema kuna dalili zote za uchokozi dhidi ya taifa hilo. Amesisitiza kwamba Urusi haihusiki na kile kilichotokea Uingereza. 

Kwenye mahojiano na shirika la habari la Utangazaji la Uigereza la BBC, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Boris Johnson ametumia maneno makali dhidi ya Urusi, akiituhumu kwa kulifurahia shambulizi hilo dhidi ya Skripal, ambalo amelielezea kama njia ya kumtisha yoyote anayempinga rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Katika hatua nyingine, waziri wa ulinzi wa Uingereza Gavin Williamson amesema serikali itawekeza kiasi cha pauni milioni 48 katika kituo kipya cha kujilinda na silaha za sumu na kuwapa chanjo maelfu ya wanajeshi wake dhidi ya ugonjwa wa kimeta.

Rais wa ufaransa Emmanuel Macron amesema anaunga mkono tathmini ya Uingereza kuwa Urusi ndio ilihusika na shambulizi dhidi ya jasusi huyo na kuapa kuchukua hatua ya kuhusiana na shambulizi hilo katika siku chache zijazo.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/AFPE/RTRE.

Mhariri:Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW