1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakamilisha ujenzi wa bomba la gesi la Nord Stream 2

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
10 Septemba 2021

Kampuni kubwa ya nishati ya Urusi Gazprom imeukamilisha mradi wa ujenzi wa bomba la gesi litakaloleta gesi nchini Ujerumani.

FLogo der Nord Stream 2 Pipeline
Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Mradi huo maarufu kama Nord Stream 2, utaongeza maradufu mauzo ya gesi ya Urusi barani Ulaya na umeiwezesha Urusi kuipiga chenga Ukraine ambayo ni hasimu wa kisiasa wa Urusi. Mkuu wa bodi ya usimamizi wa mradi huo uliokabiliwa na siasa nyingi Alexei Miller amesema ujenzi ulikamilishwa leo tarehe 10.09.2021.

Kampuni ya Gazprom ilianza ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1,200 miaka mitano iliyopita ili kupeleka gesi nchini Ujerumani, hata hivyo ujenzi ulisimama baada ya rais wa Marekani wa hapo awali Donald Trump kuweka vikwazo dhidi ya mradi huo wa dola bilioni 11. Mradi huo wa Gazprom mbili ulianza tena mwaka mmoja baadae na Urusi ilitumia vyombo vyake vya usafiri wa baharini. Kutokana na mradi huo wa Nord Stream 2 pamoja na bomba lingine, Urusi itaweza kusafirisha kiasi cha Cubic meta bilioni 110 za gesi hadi barani Ulaya kila mwaka.

Tawi la Ujerumani la kampuni ya nishati ya Urusi GazpromPicha: Jaap Arriens/NurPhoto/picture alliance

Ujenzi wa bomba hilo ulipingwa vikali na Marekani pamoja na Ukraine miongoni mwa nchi nyingine. Ukraine na Marekani zimekuwa zinaukosoa mradi huo kwa kueleza kwamba bara la Ulaya litakuwa tegemezi kwa Urusi kwa ajili ya mahitaji yake ya nishati. Ukraine pia ilikuwa inatumai kupata fedha za ushuru laiti bomba hilo lingelipitia kwenye ardhi yake.

Hata hivyo mnamo mwezi wa Julai Marekani na Ujerumani zilifikia mwafaka, zilikubaliana kwamba ujenzi uendelee lakini zitachukua hatua ikiwa Urusi itatumia nishati kama fimbo ya kisiasa dhidi ya nchi za Ulaya au ikiwa itaendelea kufanya vitendo vya uchokozi dhidi ya Ukraine. Mnamo miaka ya nyuma Urusi iliikatia Ukraine ugavi wa mafuta.

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Rais wa Urusi Vladmir PutinPicha: Mikhail Metzel/ITAR-TASS/imago images

Washirika wa Magharibi wa kampuni ya Gazprom katika mradi huo ni pamoja na kampuni za Ujerumani Uniper na Wintershall Dea tawi la kampuni ya BASF, kampuni kubwa ya mafuta inayomilikiwa na Uingereza na Uholanzi, Shell, OMV ya Austria na kampuni ya nishati ya Ufaransa Engie.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi haitaanza kupeleka gesi ya biashara kwa kupitia kwenye bomba la Nord Stream 2 hadi hapo mamlaka husika ya Ujerumani itakapotoa idhini. Ugavi unatarajiwa kuanza mnamo mwezi Oktoba.

Chanzo:/RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW