1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakanusha kushambulia kituo cha treni Ukraine

8 Aprili 2022

Urusi imekanusha shutuma kwamba imekishambulia kituo cha treni chenye abiria 4,000 wengi wao wanawake, watoto na wazee na kuuwa watu 50 mashariki mwa Ukraine, huku mbinyo wa mataifa ya Magharibi ukiongezeka.

Ukraine-Krieg
Picha: Ukrainian President Volodymyr Zelenskyy's Telegram channel/dpa/picture alliance

Wizara ya ulinzi ya Urusi imekanusha ripoti kwamba jeshi lake limehusika kwenye mashambulizi ya roketi dhidi ya kituo cha treni za abiria mashariki mwa Ukraine, ambapo mamlaka zinasema watu 50 wameuawa siku ya Ijumaa (Aprili 8).

Shirika la habari la RIA limemnukuu msemaji wa wizara hiyo akisema kwamba makombora yaliyokipiga kituo hicho, ambacho kinatumiwa kuwahamisha raia wanaokimbia mapigano, ni ya jeshi la Ukraine na kwamba vikosi vya Urusi havikuwa na shabaha zozote kwenye mji wa Kramatorsk kwa siku ya Ijumaa.

Ikulu ya Marekani imeyaita mashambulizi hayo kuwa ya kikatili ikisema picha zinazoonesha tukio hilo ni za kushitusha na kuogofya.

Msemaji wa Ikulu ya White House, Kate Bedingfield, amesema Marekani itaendelea kuiunga mkono Ukraine dhidi ya uchokozi wa Urusi.

Mashambulizi hayo yamechochea uamuzi wa Uingereza kuharakisha kutuma mitambo ya kutunguwa makombora kwa Ukraine, ikiyaita mashambulizi yenyewe kwamba "hayaingii akilini." 

Vifo vyaongezeka

Damu ikiwa imetapakaa nje ya kituo cha treni cha Kramatorsk, mashariki mwa Ukraine, baada ya mashambulizi ya roketi ambalo maafisa wanasema limeuwa watu 50 na kujeruhi wengine zaidi ya 300 siku ya Ijumaa (Aprili 8, 2022).Picha: Seth Sidney Berry/ZUMA Press Wire/dpa/picture alliance

Gavana wa mkoa wa Donetsk, Pavlo Kyrylenko, ametangaza idadi mpya ya watu waliouawa kwenye mashambulizi hayo ya leo ni 50, kutoka wale 30 waliotangazwa awali. Idadi ya waliojeruhiwa imefikia 300. 

Meya wa mji wa Kramatorsk, yalipotokea mashambulizi yenyewe, Oleksandr Goncharenko, alikiambia kituo cha televisheni ya Ukraine kwamba madaktari wapatao 40 wanashirikiana kuwatibu majeruhi, huku hospitali zikishindwa kukabiliana na idadi kubwa ya wagonjwa.

Ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu wa Ukraine inasema kiasi watu 4,000 walikuwapo kwenye kituo hicho cha treni, wengi wao wanawake, watoto na wazee wasiojiweza.

Serikali ya Ukraine imekuwa ikiwahimiza raia kuondoka eneo hilo kabla ya operesheni mpya ya vikosi vya Urusi kwenye mkoa huo.

Waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanaudhibiti mkoa mzima wa Donetsk, lakini mji wa Kramatorsk unaendelea kuwa chini ya udhibiti wa serikali ya Ukraine.

Wanadiplomasia wa Urusi waondoka Berlin

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock.Picha: Michael Sohn/AP/picture alliance

Hayo yanajiri wakati mbinyo dhidi ya Urusi ukiendelea katika mataifa ya Magharibi. Hivi leo, kundi kubwa la wanadiplomasia wa Kirusi waliofukuzwa wiki hii nchini Ujerumani wameondoka mjini Berlin.

Wizara ya Nje ya Ujerumani imesema kuwa inahakikisha kuwa maafisa hao wa kibalozi wanaondoka wote na kwa ukamilifu.

Ndege iliyowachukuwa maafisa hao 40 waliotangazwa na serikali ya Ujerumani kuwa hawahitajiki, ilituwa kwa kibali maalum mjini Berlin asubuhi ya leo kuwachukuwa.

Kwa mujibu wa mamlaka za Ujerumani, maafisa wote hao wana mafungamano ya moja kwa moja na idara za ujasusi za Urusi.

Ulaya yamrejesha balozi wake Kyiv

Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen (kulia) na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, wakiwa mji Kyiv siku ya Ijumaa (Aprili 8, 2022).Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Kwa upande mwengine, Umoja wa Ulaya umemrejesha balozi wake wa Ukraine katika mji mkuu, Kyiv, katika hatua ambayo inaashiria kuimarika kwa hali ya usalama kwenye mji huo, na ahadi ya umoja huo wenye mataifa 27 kwa taifa hilo linalovurugwa kwa mashambulizi.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, alitoa tangazo hilo leo wakati akiwa ziarani mjini Kyiv, ambako aliungana na Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, kwa mazungumzo na Rais Volodymyr Zelenksyy.

Borrell amewasifia viongozi na watu wa Ukraine kwa kusimama imara dhidi ya uvamizi wa Urusi licha ya kushambuliwa vibaya na miji yao kugeuzwa vifusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW