Urusi yakanusha njama ya kumuua mkuu wa Rheinmetall
12 Julai 2024Kampuni hiyo imetengeneza silaha muhimu ambazo Ujerumani inazipeleka Ukraine.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moscow, Dmitry Peskov amesema hawezi kutoa tamko kuhusiana na tuhuma hizo akidai kuwa ripoti iliyotolewa na shirika la habari la Marekani la CNN haiwezi kuchukuliwa kwa umuhimu kwa sababu vyanzo vyake havikuwekwa wazi.
Soma pia: Rais Putin akutana na Spika wa Bunge la Tanzania
Kulingana na ripoti hiyo ambayo kwa sasa imeandikwa pia katika gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung, maafisa wa intelijenzia wa Marekani mapema mwaka huu walifichua mipango ya serikali ya Urusi ya kumuua afisa mkuu mtendaji wa Rheinmetall Armin Papperger.
Ripoti hiyo imezusha ghadhabu Ujerumani huku waziri wa usalama wa ndani Nancy Faeser akisema serikali inakichukulia kitisho cha Urusi kwa "umuhimu mkubwa."