1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakasirishwa na Marekani kupeleka wanajeshi Poland

13 Januari 2017

Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wameanza kuwasili nchini Poland kuonyesha mshikamano na nchi washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Serikali ya Urusi hata hivyo imesema hatua hiyo inatishia usalama wa taifa lake

USA Verlegung US Truppen für Europa in Bremerhaven Timothy McGuire Kommandant für Europa
Picha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Poland imewakaribisha maelfu ya wanajeshi wa Marekani ambao waliingia nchini humo jana pamoja na vifaru na silaha nyingine nzito kwa ajili ya kutekeleza operesheni ya NATO inayolenga kuimarisha usalama wa washirika wake wa Ulaya Mashariki. Hatua hiyo imeikasirisha Urusi ambayo inasema kuwekwa kwa majeshi hayo kunatishia usalama wake.   

Baada ya miaka mingi idadi kubwa kabisa ya wanajeshi wa Marekani imepelekwa barani Ulaya. Askari 2,700 kati ya 3,500 waliwasili nchini Poland kama sehemu ya operesheni inayoitwa "Azma ya Atlantik" kwa lengo la kuionyesha Urusi kwamba Marekani inadhamiria kushikamana na washirika wake. Kamanda wa jeshi la Marekani, Kanali Christopher Norrie, alisema katika hafla ya kuwakaribisha wanajeshi wa Marekani kwamba shabaha ya kuwapeleka wanajeshi hao ni kuzuia vitisho. Naye Jenerali Jaroslaw Mika wa jeshi la Poland aliielezea siku hiyo kuwa ni siku ya kihistoria. 

Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Picture-Alliance/AP Photo/C. R. Arbogast

Hafla hiyo ilifanyika katika mji wa Zagan ulioko magharibi mwa Poland. Poland na nchi zilizokuwa chini ya himaya ya Urusi ziliomba majeshi ya Marekani na NATO baada ya Urusi kuiteka rasi ya Crimea ambayo ni sehemu ya Ukraine mnamo mwaka wa 2014 kutokana na kuhofia pilikapilika zaidi za kijeshi za Urusi katika Ulaya ya Mashariki. Urusi ambayo hapo awali iliishutumu NATO kwa kuimarisha majeshi yake katika eneo hilo, imesema kuwekwa majeshi hayo ni hatua ya kivamizi katika mipaka yake. Kuleta usasa katika jeshi la Poland limekuwa ni suala la kipaumbele kwa serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na chama cha kihafidhina cha Sheria na Haki, PiS tangu ilipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita. Msingi wa umaarufu wa serikali hiyo umetokana pia na kutoa ahadi ya kuleta usalama mkubwa. Waziri wa Ulinzi wa Poland, Antoni Mmacierewicz amesema kwamba kuwepo majeshi ya NATO kutakomesha ushawishi wa Urusi katika Ulaya Mashariki.  Kwa upande wake Urusi imejibu kwa kuweka makombora ya nyuklia katika mji wa Kaliningrad hatua ambayo wizara ya ulinzi ya Marekani imesema kuwa inayumbisha usalama barani Ulaya. Pamoja na maalfu ya wanajeshi, Marekani imepeleka vifaru zaidi ya 80 na mamia ya magari ya kijeshi ya chuma katika eneo hilo la Ulaya Mashariki. Majeshi hayo yatahamishiwa kwa zamu katika nchi za Bulgaria, Estonia, Latvia, Lithuania na Romania. Kamanda wa majeshi ya Marekani Kanali Norrie ameeleza kwamba kuwasili kwa majeshi hayo ni hatua ndogo lakini ni mfano muhimu unaoonyesha jinsi Marekani inavyoweza kujenga haraka uwezo wa kupambana kijeshi.

Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Getty Images/AFP/S. Karpukhin

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo