1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakataa kurefusha mkataba wa nafaka, dunia yalalamika

18 Julai 2023

Uamuzi wa Urusi kujitoa kutoka mkataba wa kusafirisha nafaka za Ukraine kupitia bandari za Bahari Nyeusi umezusha wasiwasi mkubwa wa kimataifa.

Ukraine | Getreideernte
Picha: Alexey Furman/Getty Images

Viongozi kadhaa wa ulimwengu wamejitokeza kuzungumzia suala hilo na taathira zinazoweza kuikumba dunia iwapo shehena ya nafaka itazuiwa na usambazaji wa chakula kutetereka.

Kumekuwa na malalamiko kuhusiana na uamuzi wa Urusi kusitisha ushiriki wake katika mkataba huo uliotoa nafasi kwa nafaka za Ukraine kusafirishwa kupitia bahari, hatua iliyosaidia kuhakikisha kwamba bei za bidhaa muhimu duniani kama ngano zinasalia kuwa nafuu.

Mapema jana Jumatatu, msemaji wa Rais Vladimir Putin wa Urusi, Dmitry Peskov, alisema kwamba Urusi itarudi kushiriki mkataba huo mara tu matakwa kuhusiana na usafirishaji wa nafaka na mbolea zake yatakapotimizwa.

Ikulu ya Kremlin hasa inataka vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi kuhusiana na masuala ya malipo, usafirishaji na bima viondolewe.

Nafaka zinahitajika mno katika Pembe ya AfrikaPicha: Felix Maringa/DW

Marekani na nchi za Magharibi lakini wamepinga madai hayo ya Urusi wakisema vikwazo vyao havilengi nafaka na mbolea za Urusi.

Guterres avunjwa moyo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema kwamba amevunjwa moyo sana kwa kuwa barua aliyomtumia rais Putin wiki iliyopita, iliyokuwa na mapendekezo ya mikakati ya kuunusuru mkataba huo, haikuzingatiwa.

Guterres amesema mkataba huo ambao ulifika mwisho rasmi jana Jumatatu, ulikuwa ni tumaini la usalama wa chakula duniani na matumaini pia katika ulimwengu ulio na matatizo chungunzima.

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan, ambaye alikuwa na dhima kubwa katika kutiwa saini kwa mkataba huo, amesema anahisi kwamba rais Putin ana nia ya kurudi kwenye mkataba huo.

Erdogan amesema atafanya mazungumzo na Putin kuelekea ziara yake inayosubiriwa kwa hamu nchini Uturuki mwezi Agosti.

Njaa kutumika kama silaha

Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, ameibua uwezekano wa kurudia usafirishaji wa nafaka bila ushiriki wa Urusi, akisema Ukraine itaomba usaidizi wa Uturuki, ili kuhakikisha kwamba vizuizi vilivyowekwa na Urusi mwaka jana, havitekelezwi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock aliyekuwa mjini New York, amemtaka rais Putin kuacha kutumia njaa kama silaha katika uvamizi wake, kwa ajili ya kupatikana amani duniani.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Shashwat Saraf ni mkurugenzi wa dharura Afrika Mashariki katika shirika la kimataifa la uopoaji IRC na amesema, athari ya Urusi kutourefusha mkataba huo zitakuwa kubwa Somalia, Ethiopia na Kenya, nchi ambazo zimekabiliwa na kiangazio kikali kuwahi kushuhudiwa katika eneo la Pembe ya Afrika katika miongo kadhaa.

Ukraine na Urusi ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa nafaka na bidhaa zengine za chakula duniani na utatizaji wa aina yoyote wa usafirishaji huo unaweza kupelekea kupanda kwa bei za chakula kote duniani.

Vyanzo: Reuters/DPAE/APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW