Urusi yakataa kurudishia Ukraine udhibiti wa kinu, nyuklia
12 Agosti 2022Konstantin Kosachev, naibu spika wa baraza la juu katika bunge la Urusi, amesema haiwezekani tena kwa Urusi kusalimisha udhibiti wa kinu hicho kwa Ukraine akisisitiza kwamba ili kuhakikisha usalama wa mtambo huo, udhibiti kamili wa Urusi unahitajika.
Kosachev aliungwa mkono na mkuu wa kamati ya bunge ya Mambo ya nje Leonid Slutsky aliyeituhumu Ukraine kwa kile alichokitaja kuwa ‘ugaidi wa kinyuklia'.
Kwenye mtandao wake wa Telegram, Slutsky amesema kauli zote za mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G7 si lolote bali ufadhili wa ugaidi wa nyuklia.
Slutsky hakutaja kwamba hali kuhusu mtambo huo ulitokana na uvamizi wa Urusi.
Vikosi vya Urusi vimekuwa vikiudhibiti mtambo huo uliopo katika eneo linalotarajiwa kukumbwa na makabiliano makali katika vita nchini Ukraine.
Urusi yaendeleza mashambulizi dhidi ya Ukraine
Nchi za Magharibi zimeitaka Urusi kuondoa vikosi vyake kwenye mtambo huo. Nao Umoja wa Mataifa ulitoa wito Alhamisi kutaka eneo la mtambo huo, liwekewe marufuku ya shughuli zozote za kijeshi.
Hata hivyo Urusi haijaonesha dalili yoyote ya kukubali kuwaondoa wanajeshi wake kwenye mtambo huo walioukamata mwezi Machi.
Ukraine imesema imekuwa ikipanga kwa wiki kadhaa mashambulizi ya kuukomboa mji wa Zaporizhzhia na mikoa jirani ya Kherson, ambayo ni eneo kubwa zaidi la himaya yake lililokamatwa na Urusi kufuatia uvamizi wake wa Februari 24.
Urusi imeweka maafisa wake wa majimbo katika maeneo hayo ikisema wanakusudia kupiga kura ya maoni kwa wakaazi wa maeneo hayo kujiunga na Urusi.
UN yataka kukagua kinu cha nyuklia cha Ukraine
Rais wa Ukraine Vollodymir Zelenskiy ameitaka Urusi kuurudisha mtambo huo mikononi mwa Ukraine akisema hilo pekee ndilo litakalowezesha udhibiti kamili na uhakikisho wa usalama wa Ulaya mzima dhidi ya hatari ya nyuklia.
Ufaransa pia ilikariri takwa hilo la Zelenskiy na kusema hatua ya Urusi kuudhibiti mtambo huo unahatarisha ulimwengu.
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia alisema ulimwengu unasukumwa katika kitisho cha maangamizi katika kiwango kinachoweza kulinganishwa na maafa ya Chornobyl yaliyotokea 1986. Ameongeza kuwa shirika la IAEA linaweza kuuzuru mtambo huo haraka iwezekanavyo.
Shirika la nishati Energoatom la Ukraine ambalo wafanyakazi wake wanaendesha operesheni ya mtambo huo chini ya usimamizi wa vikosi vya Urusi limesema mtambo huo ulishambuliwa mara tano siku ya Alhamisi ikiwemo karibu na eneo ambako vifaa vya mionzi vimehifadhiwa. Pande zote zilituhumiana kuhusika. Shirika la habari la Reuters halikuweza kuhakiki hayo kivyake.
Zaporizhhzhia: Ukraine na Urusi zatupiana lawama
Urusi inadai Ukraine inafyatua hovyo risasi dhidi ya mtambo huo. Nayo Ukraine inadai wanajeshi wa Urusi ndio waliushambulia na wanatumia mtambo huo kama ngao wakati wakishambulia miji jirani inayoshikiliwa na Ukraine.
Mnamo Alhamisi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kujadili hali hiyo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizitaka pande zote mbili kuacha vita karibu na mtambo huo.
Kwenye mkutano huo, Marekani iliunga mkono wito wa kutaka shughuli za kijeshi zisifanyike karibu na mtambo huo na imelihimiza shirika la kimataifa linalosimamia nguvu za atomiki IAEA kuuzuru mtambo huo kwa uchunguzi.
(RTRE;DPAE)