1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakiri kupoteza zaidi ya wanajeshi 60

3 Januari 2023

Urusi na Ukraine zimeendelea kushambuliana vikali huku Urusi ikikiri kupoteza wanajeshi wake zaidi ya 60 na Ukraine ikisema imegundua kile inachosema ni "kambi za mateso" kwenye mji wa mashariki wa Kharkiv.

Ukraine Kharkiv Region Front Artillerie
Picha: Evgeniy Maloletka/AP Photo/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Katika tukio la nadra, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kwamba wanajeshi wake 63 waliuawa kwenye Mkesha wa Mwaka Mpya baada ya mripuko kuharibu kambi ya muda kwenye chuo kimoja cha amali katika mji wa Makiivka, mashariki mwa Ukraine. 

Mapema, Ukraine ilisema wanajeshi wa Urusi waliouawa kwenye mashambulizi hayo walikuwa 400 na waliojeruhiwa ni 300, idadi ambayo Urusi imeikanusha ikisema imetiwa chumvi. 

Wakosoaji wa Urusi wanasema wanajeshi hao walikuwa wamejihifadhi pamoja na shehena ya silaha ambayo wizara ya ulinzi wa Urusi wanasema ilishambuliwa kwa makombora manne yaliyorushwa kutoka mitambo iliyotengenezwa Marekani. 

Wanablogu za kijeshi nchini Urusi wanasema kiwango cha madhara yaliyotokana na mashambulizi hayo kimetokana na silaha zilizowekwa katika jengo lile lile ambalo makamanda walijuwa kuwa linaweza kufikiwa na maroketi ya Ukraine.

Mashambulizi hayo ya Makiivka yalifanyika wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi yake makali ya ndege zisizo rubani dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Mashambulizi hayo pia yalielekezwa kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Ukraine katika mkoa wa Donetsk.

'Kambi za mateso' zagunduliwa

Katika mji uliokuwa unashikiliwa na Urusi na ambao sasa umekombolewa wa Kharkiv, jeshi la Ukraine lilisema limegundua maeneo 25 ambayo yalikuwa kambi za mateso.

Makaburi ya pamoja kwenye mkoa wa Kharkiv.Picha: AFP

Kwa mujibu wa jeshi hilo, wanajeshi wa Urusi walitumia kambi hizo kuwashikilia na kuwatesa raia katika mazingira yasiyo ya kibinaadamu.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Volodymyr Timoshko, aliandika kwenye ukurasa wa Facebook kwamba baadhi ya wafungwa waliteswa kwa kutumia umeme na kuvunjwa viungo vyao.

Wanajeshi wa Urusi walikuwa wamelikalia eneo hilo kwa miezi kadhaa na kulazimika kujiondowa mwezi Septemba baada ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka jeshi la Ukraine.

Tangu wakati huo, miili 920 ya raia, ikiwemo ya watoto 25, imeshagunduliwa katika eneo hilo lililokombolewa na, kwa mujibu wa Timoshko, wote waliuliwa na wanajeshi wa Urusi.

Uchunguzi wa mamlaka za Ukraine unabainisha kuwa vikosi vya Urusi vimehusika na uhalifu wa kivita kwenye maeneo vilivyokuwa vinayashikilia.

Miongoni mwa matukio hayo ni kugunduliwa kwa miili ya watu zaidi ya 400, wengi wao wakiwa wamekufa vifo vya mateso.

Uchunguzi bado unaendelea.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW